Ni saa mbili kamili za Asubuhi ndani ya hoteli moja maarufu ndani ya makao makuu ya nchi mjini Dodoma ,ndani ya chumba kikubwa cha hadhi ya juu ndani ya hoteli hii , anaonekana mzee mmoja mweupe mwenye nywele nyingi kichwani , lakini zilizokuwa na mvi ,Mzee huyu kwa makadirio ya umri hakuwa chini ya miaka Hamsini.
Mzee huyu alikuwa amesimama huku nyuma yake kwenye kitanda alionekana mrembo mmoja maarufu nchini akiwa amelala , akiwa hana habari na kinachoendelea kwa mgoni wake.
Mzee huyu alikuwa ameshikilia simu , lakini simu ilionekana nzito kwake , kwani alikuwa ni mwenye kutetemeka sana,Mzee huyu wakati akiendelea kuangalia simu yake , mara simu yake ilipata uhai na kuanza kuita na mzee huyu kinyonge sana aliipokea.
“Nini kimetokea Hassani , inakuwaje mwanangu akauwawa kikatili namna hii”
“Mzee hata sisi tumeshindwa kuelewa na swala hili tunaendelea kulichunguza kwanini limetokea ghafla hivi”
“Naomba hili lifanyike haraka Hassani , inaniuma sana kumpoteza Karim mrithi wangu”
“Sawa Mzee , swala hili lazima tutalichimba kujua undani wake nakuhakikishia lazima tulipize kwa aliemfanyia unyama huu Karim”Ilisikika sauti hio na mzee huyu alikata simu , huku akisogelea sofa lililokuwa pembeni kwa kujikokota huku akiwa amejishika kifua chake , mzee huyu alionekanna kuwa katika maumivu ya kumpoteza kijana wake.
Alichukua mvinyo uliokuwa kwenye chupa na kumimina kwenye glass na kunywa kwa pupa na kisha akarudisha glasi kwenye meza.
“Naapia kwa mbingu na Arfhi uliehusika na kifo cha mwanangu nitakusaka mahali popote na nitahakikisha na kukata kiungo kimoja kimoja mpaka kifo chako”.Aliongea mzee huyu huku akiegamia kwenye sofa na kufumba macho kwa sekunde lakini alikuja kushituliwa na simu ilioanza kuita mfululizo , baada ya kuangalia nani anampiga aliona ni mke wake na hapa ni kama mzee huyu alizinduka kwani haraka sana alikimbilia nguo zake na kuvaa.
“Sijui mke wangu ataipokeaje hii taarifa”Aliwaza mzee huyu huku akiangalia simu ambayo ilikuwa ikiita kwa mara ya pili , lakini hakupokea Zaidi ya kutoka ndani ya chumba hiko.
Naam huyu ni meya wa mji wa jiji hili la Dodoma afahamikae kwa jina la Bakari Juma lakini pia anafahika kama “The man behind the Power’ndani ya kundi la The Black Mamba.
****
Juma aliamka asubuhi na mapema sana kama kawaida yake , ili awahi kwenye kazi yake ya ubeba mizigo , siku hii bwana huyu alionekana kuwa na furaha sana , kwani kila akikumbuka tukio la jana moyo wake ulikuwa mweupe.
Baada ya kujiandaa alimuaga Najma na kuianza safari ya kuelekea kazini ndani ya mdakika kadhaa tu alikuwa ashafika na kupata dili la haraka na kulishughulikia.
Muda wa saa mbili ndani ya soko hili kulikuwa kumechangamka sana na kama ujuavyo Mbagala kwa kuwa na watu wengi ,Juma akiwa anapiga hadhithi na wenzake ndipo alipoanza kusikia habari ambazo hakuwa amezitarajia.
“Oy wadau inasemekana Karim amekufa jana kwa kuuliwa”Aliongea Yusuph na kumfanya Juma ashangae na kuona huenda Yusuph amechanganya majina kati ya Karim na Roma.
“Wee..! kweli acha utani ,ilikuwaje?”
“Mwamba nasikia kagusa pasipo gusika na hivyo kuingia kingi”
“Oy yusuph ni kweli Karim kafariki?”
“Habari ni za kweli kabisa , japo kwa sasa ni za chinichini ia , mwili wa Karim upo Muhimbili ninavyoongea hapa na hakufa peke yake”Kwa muonekano wa Yusuph wa uongeaji wake Juma aliamini bwana huyu hakuwa akidanganya kwani alikuwa akimwamini sana , lakini bado kwenye kichwa chake alikuwa na maswali ni kwa namna gani Karim amekufa na sio Roma , au watu wameona vibaya hayo ndio yaliokuwa mawazo yake.
Juma aliendelea kuchapa kazi mpaka muda wa saa tano na hapo ndipo aliposikia simu yake inaita na kuitoa mfukoni na namba ilikuwa mpya.
“Juma!!, Najma hali yake mbaya rudi umuone mdogo wako”Juma mara baada ya kusikia sauti hii aliitambua vyema kama moja ya wanawake waliokuwa ni wapangajii katika nyumba yao na Juma hakutaka kubaki ndani ya hili soko kkwani aliondoka haraka na kurudi nyumbani.
Ni kweli mara baada ya kuingia ndani ya chumba cha Najma alimuona dada yake alivyokuwa akitoa jasho jingi , huku hali yake ikiwa mbaya , ule weupe aliokuwa nao Najma ulikuwa umebadilika na kuwa mwekundu , huku mwanadada huyu akitetemeka.
Juma hali ile ilimuogopesha na maamuzi alioyafanya haraka haraka ni kumchukua Najma na kuita bajaji kwa ajili ya kuelekea hosputalini akishirikiana na mpangaji aliempigia simu.
Ndani ya madakika kadhaa tu walikuwa washafika ndani ya hospitali ya Zakhiem na kupokelewa , huku Najma akiingizwa kwenye chumba cha daktari pamoja na Juma.
Juma alitoa maelekezo ya haraka haraka huku akiingiza maeneno mengi yasio na ukweli na kisha dokta huyo aliandika vipimo na Najma akatolewa na kuingizwa wodini .
Zilikuwa ni dakika kadhaa tu za Juma baada ya kutoa maelezo kwa dokta na kumuacha mpangaji aendelee kumwangalia Najma kutokana na yeye kutoruhusiwa kuingia wodi za wanawake , alitoka nje kabisa ya geti na wakati anatoka tu ni kama alikuwa akisubiriwa kwani , vijana wawili waliovalia mavazi ya kawaida walimsogelea.
“Oy Broo wewe ndio Juma?”
“Yes ni mimi”.
“Kuna inshu Fulani tunataka kukuuliza , ila hapa si salama tuna gari yetu upande wa pili itakuwa vyema kama tutaenda wote”Juma alifikiria kwa muda huku akiwangaalia vijana hawa na kuona hawakuwa na hatari yoyote kwake na aliona ni vyema kuongozana nao.
Gari walikuwa wameipaki upande wa kushoto mbele kabisa na ukumbi maarufu jijini Dar es salaam unaofahamika kama Dar Live , vijana wale waliisogelea gari nyeupe aina ya Toyota Corola na kisha mmoja aliingia wa kwanza na kisha akafatia juma na yule mwingine akaingia mbele.
Kitendo cha juma kuingia tu kwenye gari alishituka akiwekewa kitambaa kwenye pua zake na mtu ambaye ilionesha ni Dhahiri kabisa alikuwa ndani ya gari hili kabla ya Juma kuingia.
Baada ya ukio lile lililofanyika bila ya mtu yoyote kuona kinachoendelea hatimae gari ile ilitolewa kwa spidi kueekea upande wa kariakoo na ikawa Juma katekwa kiulaini.
****
Roma kama kawaida alifika kazini huku kwenye akili yake akiwa na mawazo ya kwenda kupoteza poteza muda kwa kucheza magemu ili arudi zake nyumbani kula na kwenda kiwanja cha bata.
“Hiii kazi nafanya kumridhisha tu Edna , ila kutokana na ugonjwa wangu sipaswi kufanya kazi ambayo inanifikirisha , lazima nijichunge”Alijiongelesha Roma wakati akiingia ndani ya ofisi yake ya kazi.
Na siku hii haikueleweka , ila Wafanya kazi walionekana kuwa bize kweli na kazi na hata Roma alishangaa kwani hata Recho ambaye alikuwa akipenda kuongea sana , alionekana kuwa bize na Zaidi ya salamu hakukuwa na Zaidi ya maongezi, ila Roma hakujali sana yeye aliendelea zake na kucheza gemu.
Muda wa chakula ulivyowadia ndio alikuwa mtu wa kwanza kuinuka kwa ajili ya kuelekea kula kitendo kilichowafanya wawafanya kazi wenzake wamwangalie , ila hakujali , kwani Roma sifa yake kubwa ni kwamba jamaa huyu mshipa wa Aibu ni kama umekatwa.
Roma baada ya kujiona ameshiba , alimkumbuka Doris sana na alitamani amuombe mchezo baadae , ila alikumbuka kuwa alikuwa amenuniwa tokea tukio la yeye kulala na waziri Neema Luwazo , hivyo hakutaka kujihangaisha kwake , aliona kama Neema atarudi kwake basi wataendelea na kama hatorudi hana haja ya kwenda kuomba msamaha na kubembeleza.
Roma baada ya kushiba alichuku maji yake ya Kilimanjaro makubwa na kisha alitoka sehemu hii ya kantini lakini ile anakata kulia ili kuingia upande ambao zipo Lift alikuja kukutana na Edna njiani akiwa na Doris , walionekana walikuwa ndio wanaelekea kula ,Doris hakuongea na Roma na hivyohivyo hata kwa Edna , alimpita Roma kama hamjui , ila kwa Roma hakujali licha ya kujisikia vibaya moyoni.
Ilikuwa ni muda wa saa kumi za jioni Roma akiwa ndani ya sehemu ya kuegeeshea magari , akilisogelea gari lake V8 , mara gari aina ya BMW M4 ya pink ilikuja kupaki pembeni yake kiasi kwamba ilitaka kumgonga.
Roma wakati akishangaa , kioo cha gari hio kilishushwa na kumuona mwanamke mrembo na huyu hakuwa mwingine bali aalikuwa ni Nasra.
“Roma naomba unisindikize mahali?”Ilisikika sauti ya mrembo huyu na Roma alimwangalia huyu mwanadada na kisha aliitikia kwa kichwa na kuingia kwenye gari ya huyu mrembo na kisha ikatolewa ndani ya jengo hili kwa spidi.
Gari hii haikwenda mbali sana , kwani ilikuja kusimama nyuma ya hospitali ya Aghakhani ,Baada ya gari hii kusimama mwanadada Nasra alishuka kwa maringo na Roma nae alishuka na mwanadada huyu alielekea upande wa Beach, chini kidogo sehemu ambao ilikuwa na miti.
“Nasra yuko wapi?”Ilikuwa ni sauti ya Roma akimwangalia mwanadada aliekuwa mbele yake , swali hilo ni kama lilikuwa la kijinga kwani mtu aliekuwa mbele ya Roma alikuwa ni Nasra , lakini sio kweli kwani baada ya Roma kuuliza swali hilo mara mwanadada yule alibadilika sura na kuwa mtu mwingine kabisa ,Alibadilika kama Jini.
Alikuwa ni mwadada wa kijapani mrefu saizi ya kati. Mwenye mwili mwembamba na ungejiuliza ni kwa namna gani mwanadada huyu aliweza kuchukua muonekano wa Nasra mfanyakazi wa kampuni ila huo wote ni uchawi wa kijapani.
“Yamata sect ! Naona wajapani mmezidi kuimarika kwenye mbinu yenu ya kichawi ya kuiba uhusika wa mtu”Aliongea Roma kwa lugha ya kijapani.
“Tunazo mbinu nyingi za kichawi Hades , ambazo ni mpya na hauzitambui”.Roma alitabasamu na kumwangalia mwanamke huyu wa kijapani akimwita Hades.
“Jina lako ni nani kabla sijakuua”Aliongea Roma.
“Jina langu ni Tanya na nipo hapa Tanzania kwa aili ya kuchukua jiwe la Kimungu(Godstone)”Roma alitabasamu na hapo hapo akakumbuka kiboksi alichokuwa amekificha kule nyumbani kwenye chumba cha mazoezi , alikumbuka pia siku ambayo alisachiwa kule nyumbani kwa Juma alikokuwa amepanga , aliweza pia kukumbuka siku ambayo anaenda ikulu na Edna kuna gari iliokuwa ikiwafatilia nyuma.
“Inaonekana mpo hapa nchini kwa muda mrefu kidogo kuliko nilivyowadhania”.
“Umepatia tupo hapa nchini kwa Zaidi ya mwezi sasa na , tumekuwa tukikufatilia kwa kila unachokifanya kila siku , lakini Master anahitaji jiwe la kimungu mapema na hataki tena tukiongeza hata siku moja hapa nchini , hivyo leo utaniambia ni wapi jiwe hilo lilipo”
“Sijui mnacho kiongelea kwani sina jiwe hilo na hata kama ningekuwa nalo nisingewapatia”
“Unajidanganya Hades, Nasra yupo mikononi mwetu na kama unataka aishi huna budi kutupatia kile tunachotaka”
Aliongea Tanya mwanadada huyu wa kijapani akimwita Roma Hades , yaani Mungu wa wafu au Mungu wa wahalifu na jina hili linatoka katika historia ya Ugiriki ya kale.
Roma alimwangalia Tanya na kuona huyu mwanadada hakuwa akitania hata kidogo , lakini licha ya hivyo hakuwa tayari kutoa Jiwe alililokuwa nalo kwani alihofia nguvu ya jiwe hilo endapo likitua kwenye mikono ya watu ambaoo sio sahihi dunia inaweza ikawa sio salama na hata mtu aliemkabidhi jiwe hilo alikuwa na maana kubwa kani aliamini kwamba Roma ndio mtu pekee ambaye ana uwezo wa kulilinda lisiwafikie wahalifu..
Roma hasira zilianza kuonekana kwenye macho yake , na kiini cha macho yake kikaanza kubadilika rangi na kuwa cha kijani , tena kijanni kilichokolea kiasi kwamba kilianza kumuogepesa mwanadada huyu wa kijapani.
“Hades ukifanya ujinga Nasra atakufa , yupo kwenye mikono yetu na sipo hapa kwa ajili ya kupigana”
“Mpaka kunileta mahali hapa ni Dhahiri upo kwa ajili ya kupigana na hata haupo hapa kwa ajili ya kupigana umevunja sharia kuu mbili nilizoweka , sipendi kutishiwa na pili sipendi mtu anaetumia watu wengine kunipata”Baada ya kusema hapo Roma kama upepo alitoweka sehemu aliokuwa amesimama na kumsogelea Tanya ,lakini ile anafika ile sehemu Tanya alipotea ghafla na hapa Roma alitabasamu.
“Kajinga sana haka kademu , kanaona kwa vijimtego vyake vya kichawi kanaweza kunizidi hakuna mchawi aliewahi kunizidi”Aliwaza Roma na kisha alifumba macho huku masikio yakiwa juu juu kama popo na hapa alionekana alikuwa akipambana kwa hisia kwani , sekunde chache tu alikuwa ashahama aliposimama na kwa spidi ya ajabu alirusha ngumi na kilichosikika ni:
“Aiii...”.Na hapa mwanamke yule alijitokeza kwa mara nyingine.
“Leo nakuua hapahapa”Aliongea Roma huku akianza kupeleka mashambulio kwa kasi , yaani kwa namna wawili hawa walivyokuwa wanapigana kama ungekuwepo eneo la tukio ungehisi upepo tu ambao sio kawaida.
Tanya aliruka hewani huku akija upande aliosimama Roma kwa spidi ya hali ya juu , na ile anamkaribia karibu alirusha kisu ambacho alimlenga nacho kwenye koo la shingo , lakini tendo hilo Roma aliliona na alichofanya ni kuruka juu na kisha akazuia kile kisu kwa mkono kiasi kwamba kikaenda kutua kwenye mchanga wa baharini , baada ya kutua Roma kwa spidi ya hali ya juu alikichukua na kumrushia Tanya , lakini mwanadada huyu alionekana mwepesi balaa kwani alijibiringisha hewani mara mbili na kupotea , lakini kwa upande wa Roma ni kama vile alitegemea kitendo hicho kwani ile Tanya anapotea alisogea upade wa kushoto na kurusha ngumi nzito na mguno wa kike wa maumivu ulisikika na Tanya alikuwa chini , ngumi ile ilionekana kumtaiti vyema , Roma hakuishia hapo tu alimsogelea na kumshika koo.
“Niambie Nasra yuko wapi kabla sijakuvunja shingo”Aliongea Roma kwa sauti kama ya Roboti , sauti ambayo ilimuogopesha Tanya lakini kabla Tanya hajavunjwa shingo mara gari nyingine ilifika na wakashuka watu wawili kwa haraka sana na kusogelea uande aliokuwepo Roma.,wote walikuwa wanaume pia wakiwa wajapani.
“Naona wenzako wamefika na hii inanirahisishia kazi , nitawaua wote hapa hapa”Aliongea Roma huku akijiandaa kumvunja shingo Tanya .
“Hades Acha usimuue tupo tayari kukupatia Nasra”Aliongea mwanaume yule wa kijapani kwa lugha ile ile ya kijapani na Roma alimwangalia na kisha kuwajibu kwa kijapani.
“Siwezi kuwaamini”.
“Nasra yupo kwenye gari , unaweza kumchukua Tanya mpaka kwenye Gari na ukithibitisha kwa kumuona Nasra tunaomba umuachie”
“Nikora niko tayari kufa , ila hakikisheni tunapata jiwe na mumpelekee Master”
“Hapana Tanya Master alitupa maagizo ya kukulinda kwa namna yoyote ile”Aliongea huyu jamaa ambaye Tanya alimwita kwa jina la Nikora.
Roma aliona afanye kama walivyokuwa wanataka na alimchukua Tanya kama mateka na kwenda nae kwenye gari , na akafungua mlango na kumuona Nasra akiwa hajitambui huku akiwa hana nguo hata moja.
Baada ya kujiridhisha , Roma alimpiga Tanya ngumi na mwanadada huyu alitoa ukulele na baada ya kuridhika Roma alimsukuma kwa nguvu na kwenda kutua kwenye mchanga wa Beach na kitendo hiki kuna baadhi ya watu waliokiona ,ila walikuwa bize na mambo yao.
Roma alitoa gari ya Nasra na kwenda kuisimamisha kwenye duka moja la nguo ,alinunua nguo za kike na kurudi nazo kwenye gari na kulitoa kurudi kwenye kampuni , baada ya kuingiza gari sehemu ya maegesho alimshika kwa kumuwekea Nasra kiganja cha mkono kwenye kifua na akashituka.
Nasra alijishangaa akiwa uchi pembeni ya Roma , alimwangalia Roma huku akionekana ni mwenyekuchanganyikiwa na kitu cha kwanza kuziba ni sehemu zake za siri , lakini Roma wala hakujali alikuwa ametabasamu tu akimwangalia mwanadada huyu anavyoona aibu.
Comments