"Vipi, wapi unaelekea?" aliuliza mwanaume yule.
"Naelekea Posta."
"Okey, ingia twende. Naelekea upande huo, nina baadhi ya maswali nataka nikuulize," aliongea jamaa yule, jambo lililomfanya hata Damiani ashangae—inawezekanaje mtu asiyemjua awe na maswali ya kumuuliza? Fikira hiyo ilimpa mashaka mengi kuhusu mtu huyo.
"Fanya haraka, ingia acha uoga. Asubuhi yote hii unawaza mambo mabaya," aliongea yule jamaa, kana kwamba alijua ni nini Damiani alikuwa akimaanisha. Kwa mashaka mengi, Damiani aliingia kwenye gari hilo, ambalo liliwashwa na kuondoshwa eneo hilo.
"Unaenda kufanya interview?" aliuliza yule bwana, jambo lililomshangaza Damiani zaidi—ni vipi mtu huyu alijua kuwa anaenda kwenye interview?
"Usiwe na wasiwasi, nimeishi miaka mingi na najua hulka ya vijana wengi, hasa wanaoenda kuomba kazi. Wewe kwa uvaaji wako unaonekana wazi unaenda kufanya interview, kama siyo kuomba kazi."
"Yeah! Naenda kufanya interview," Damiani alijibu.
"Umesomea kozi gani na elimu yako ni kiwango gani?"
"Degree of Finance and Accounting in Public Sector."
"Okey, safi na hongera. Unapaswa kujiamini tu. Maswali wanayouliza ni ya kawaida sana. Unaweza kuulizwa hata 'elfu kumi ina mnyama gani?' na ukakuta swali lina maksi nyingi," aliongea yule bwana huku akiongeza umakini katika barabara iliyokuwa na magari mengi asubuhi hiyo.
Hawakuchukua muda mrefu walipofika Posta. Gari liliishia kusimama mbele ya jengo la Waterfront, na Damiani akashuka. Bado alikuwa na maswali mengi kichwani mwake kuhusu yule jamaa—kwa nini alisema kuwa ana maswali ya kumuuliza lakini hakumuuliza hata moja? Alishangaa lakini hakutaka kufikiria sana. Huenda jamaa huyo alitaka tu kumpa lifti na kumsaidia, kama alivyosema kuwa alijua Damiani anaelekea kwenye interview.
Alipokuwa akitembea kuelekea Samora, alikumbuka yale maneno ya jamaa huyo: "Unaweza kuulizwa hata 'elfu kumi ina mnyama gani?'" Hapo ndipo Damiani alipoanza kujiuliza—elfu kumi ina mnyama gani? Alijaribu kufikiria kwa makini lakini hakuweza kupata jibu. Aliinua mkono wake na kuangalia saa yake, akagundua bado ana muda wa kutosha kabla ya interview kuanza.
Akiwa njiani, aliamua kusogelea duka moja la Tigo Pesa ili kutoa kiasi kidogo cha pesa kwa ajili ya mahitaji yake ya siku hiyo, na pia kuhakikisha anakuwa na nauli ya kurudi nyumbani kwao Lushoto.
"Kumbe tembo! Daah! Upuuzi kabisa… yaani siku zote naishika hii hela lakini sijawahi kugundua kuwa mnyama ni tembo," aliongea huku akivuka barabara.
Baada ya kutembea hatua chache, aliona jengo alilokuwa akilitafuta kwa umbali wa mita kadhaa. Ndani ya jengo hilo ndipo kampuni ya usafirishaji aliyokuwa akitafuta na kwenda kufanya interview ilipokuwa.
Alipofika ndani, alipatwa na mshangao—kulikuwa na watu wengi waliokusanyika, wote wakiwa wameitwa kwa ajili ya kufanya interview.
"Hapa kweli kuna nafasi ya kupata ajira?" alijiuliza kimoyomoyo huku akiingia ndani kabisa ya jengo hilo na kuelekea mapokezi.
Aliambiwa kuwa utaratibu ni kusubiri kwani interview itaanza muda si mrefu. Alijiunga na wenzake, akijipa moyo na kukumbuka kwamba kwenye nafasi yoyote ya kuchaguliwa, hakuna sababu ya kukata tamaa. Alikuwa amejiandaa vya kutosha, hivyo aliendelea kujiweka tayari kwa interview.
Baada ya takribani dakika arobaini, walitangaziwa kuwa interview imeanza. Ilikuwa ni written interview (mahojiano ya maandishi) kwa nafasi ya Finance Manager (Msimamizi wa Fedha).
Mameneja wa rasilimali watu waliokuwa wakisimamia interview hiyo walitoa taratibu na maelekezo ya kila namna, kisha interview ikaanza. Cha ajabu kwa Damiani ni kuwa jambo lile aliloambiwa na yule mtu aliyempa lifti lilijirudia—aliulizwa swali lile lile: "Elfu kumi ina mnyama gani?"
Ilikuwa bahati ajabu! Damiani alijikuta akishangaa ni kwa vipi yule mtu alijua kwamba swali hilo litaulizwa.
Interview ilikwenda vizuri kwa upande wake, na aliamini kuwa alikuwa amefanya vizuri. Kilichobaki sasa ni kusubiri matokeo. Japokuwa alikuwa na mashaka na yule mtu wa asubuhi, alijikuta akiona kama jamaa huyo alikuwa malaika wake aliyekuwa ametumwa na Mungu.
Upande Mwingine…
Ndani ya jengo la LPPF Tower, lililopo Mikocheni Sayansi, gari moja nyeusi aina ya Range Rover Sport ilisimama katika eneo la maegesho.
Mwanaume mmoja mwenye umri wa takribani miaka hamsini alishuka. Alikuwa amevalia suti nadhifu iliyomkaa vizuri. Mwili wake ulikuwa mkubwa kiasi, na afya yake ilionekana kuwa nzuri. Aliambatana na mwanaume mwingine aliyevaa miwani, ambaye kwa haraka haraka alionekana kuwa mlinzi wake au msaidizi wake.
Waliingia ndani ya jengo hilo, huku yule mzee akiwa ameshikilia miwani yake ya jua mkononi, wakati msaidizi wake akiwa amebeba briefcase nyeusi. Walipofika kwenye lifti, walibonyeza kitufe cha namba 16, wakisubiri kufika ghorofa waliyokuwa wakielekea.
Walipotoka kwenye lifti, walitembea kwenye korido ndefu yenye mandhari ya kuvutia. Mwisho wa korido hiyo, kulikuwa na maandishi yaliyoandikwa:
KIMBONA INTERNATIONAL LINK AND COMPANY (KILAC)
Yule mzee alitembea kwa mwendo wake wa taratibu lakini wenye afya, mpaka alipofika mapokezi. Mbele yake, alisimama dada mmoja aliyekuwa amevalia nadhifu kabisa.
"Shikamoo, boss. Karibu kazini," aliongea kwa heshima kubwa.
Mzee huyo alijibu kwa sauti isiyoonyesha kujali sana, kisha akaendelea kuelekea ofisi moja iliyoandikwa Mkurugenzi. Alipoingia, yule msaidizi wake aliweka ile briefcase juu ya meza.
Ofisi hiyo ilikuwa ya kuvutia sana, ikiwa na samani za kifahari zilizoongeza uzuri wa mazingira yake.
"Okey, Derick, tutaonana baadaye. Hakikisha unafuatilia lile suala kwa umakini mkubwa. Baadaye nina kikao, nataka kuwa kwenye nafasi nzuri kwa ajili ya kikao hicho."
"Sawa, boss," alijibu yule kijana kwa sauti ya kikakamavu, kisha akatoka ndani ya ofisi hiyo.
Dakika kumi baadaye, simu iliita—ilikuwa ni kutoka kwa secretary wake, akimjulisha kuwa kuna mgeni wake. Mzee huyo aliruhusu mgeni huyo kuingia.
"Mister Kimbona!"
"Samuel! Hahaa… Umefika lini Tanzania?"
Mister Kimbona aliongea kwa bashasha sana huku akimlaki mwanaume huyo aliyeingia ofisini mwake…
Alikuwa ni mwanaume wa saizi yake, si mrefu sana, na umri wake ulikadiriwa kuwa miaka arobaini hivi. Alikuwa amevalia suti yake ya gharama ya rangi ya buluu.
"Nimefika juzi mara baada tu ya kupata taarifa za kunifurahisha moyo wangu."
"Hahaha, karibu sana! Unipe hizo taarifa, huenda na kwangu pia zikawa za kufurahisha."
"Wewe ushazisikia sana, na kama ni za kufurahisha basi zishakufurahisha mpaka zikachuja."
"Hahahahaha... hahaha... ni kweli kabisa usemayo, na najua ni kipi unamaanisha hahaha... Karibu sana Tanzania kwa mara nyingine kwenye nchi yako."
Watu hao wawili walionekana kuwa maswahiba wakubwa. Nyuso zao zilionyesha furaha, na walionekana kufurahia jambo fulani.
"Nimekuja Tanzania kwa kazi maalum. Naamini unaelewa jinsi biashara zetu zilivyoyumba ndani ya utawala wa mwendazake. Sasa baada ya kusikia kuwa keshatutangulia mbele za haki, kwangu ilikuwa taarifa njema sana. Nimeona huu ni wakati mwingine wa kufufua biashara zetu."
"Ni kweli usemayo, lakini sidhani kama itakuwa rahisi au jambo la kufanyika haraka haraka. Linahitaji connection, na unajua nchi yetu imeimarika kiusalama kwa sasa."
"Ndiyo, hilo nalifahamu fika, na ndio maana nikasema nimekuja kwa kazi hii. Mtu ninayemuamini kusaidia katika mpango huu ni wewe. We have to establish our destroyed system once again."
"Nimekusikia na ninaelewa shauku na mipango yako, lakini mimi nakusaidiaje katika hilo?"
"Nafikiri unaelewa kuwa Mister Bruno ndiye alikuwa chanzo cha mfumo wetu kufa hapa nchini mara baada ya mwendazake kuchukua madaraka."
"Ndiyo, nalielewa fika suala hilo."
"Sasa hapo ndipo tunapoanzia."
"Kivipi, Sam??"
"Come on, Kimbona! Usiniambie siku hizi umekuwa mlokole kiasi cha kushindwa kung'amua suala dogo kama hili."
"Haha… you mean to kill him??"
"Correct! Na naamini hilo ni jambo unaloliweza sana na lipo ndani ya uwezo wako. Naujua upande wako mwingine, na ikiwa utauitumia vyema, tutafanikiwa. Nakwambia, mtu wa kwanza kufaidi si mimi tu, bali ni wewe pia. Utakuwa sehemu ya mfumo." Aliongea mwanaume huyo anayejulikana kwa jina la Samueli kwa lafudhi iliyochanganyika na tamathali za lugha za nje.
Bwana Kimbona alijikuta akiwaza, akakuna kichwa, kisha akainua uso wake na kumwangalia Sam usoni kabla ya kuachia tabasamu.
"Assume it's done from now on. We are back, my friend," alisema huku akimfanya Sam kufurahia sana. Kisha walipigiana mikono na kutakiana siku njema, huku Sam akimsisitizia kuwa suala hilo lifanyike mapema.
******
Katika kundi la watu waliokuwa wakitoka wakiwa na tabasamu, mmoja wao alikuwa kijana aitwaye Damiani. Wenzake wengi walikuwa na nyuso za kukata tamaa kwa kile walichokutana nacho.
"Dah! Nimetumia pesa zangu zote kusoma, lakini leo nimeshindwa kung’amua elfu kumi ina mnyama gani! Hata hawa HR wenyewe wanazingua," alisema kijana mmoja kwa sauti ya malalamiko, akiwa amezungukwa na marafiki zake.
Swali hilo lilikuwa gumu na halikutarajiwa, hasa kwa nafasi kama hiyo ya finance manager (msimamizi wa fedha). Hakukuwa na kijana mmoja tu aliyelalamika, bali wengi walionyesha kuchukizwa na aina hiyo ya swali. Lilichowaudhi zaidi ni kwamba maswali magumu kama hilo yaliwekewa maksi chache.
"Mambo!"
Sauti nyororo ilisikika na kupenya kwenye ngoma za masikio ya Damiani, ikimfanya ainuke kutoka pale alipokuwa ameegemea uzio akitazama magari yanayopita na watu waliokuwa kwenye hekaheka za siku hiyo.
Aligeuka na kumwona msichana mrembo kweli kweli. Alikuwa mrefu, saizi ya kati, mwenye rangi iliyodhihirisha kuwa ni mchanganyiko wa mataifa mawili. Kwa haraka haraka, mtu angeweza kudhani kuwa alikuwa nusu Mhindi au Mzungu na Mwafrika. Uso wake ulipambwa na tabasamu, likiongeza uzuri wa vishimo vya mashavu yake.
"Poa, mambo?" aliitika kwa uoga uoga.
"Naitwa Merina, wewe je?"
"Damiani."
"Ohoo! Na wewe upo kwenye interview?!"
"Ndiyo."
"Hata mimi pia! Nafurahi kukufahamu, Damiani," alisema msichana huyo kwa uchangamfu.
"By the way, how was the written test?" aliuliza Merina, akimfanya Damiani atabasamu kidogo kabla ya kujibu.
"Nashukuru Mungu, ilikuwa safi. And you?"
"Me pia."
Jibu hilo lilimfanya Damiani awaze. Kama msichana huyo amefaulu kujua elfu kumi ina mnyama gani, basi nafasi yake ya kuchaguliwa inapungua.
"Umetokea chuo gani?" aliuliza Damiani.
"Harvard."
Jibu hilo lilimfanya Damiani ashtuke kidogo, kwani alijua Harvard ni moja ya vyuo vikuu maarufu duniani, kilichopo Marekani.
"You mean USA?" aliuliza kwa mshangao.
"Yeah!"
Hapo ndipo Damiani alipoishiwa nguvu kabisa. Kama msichana huyo alikuwa amepatia maswali yote ya written test, basi hata kama yeye atapita na kwenda kwenye oral interview, asingefua dafu mbele yake.
"Congratulations!" alisema kwa unyonge.
"Thanks! And you?"
"TIA."
"Ooh! Kipo wapi?"
"Tanzania Institute of Accountancy. Kipo njia ya Mbagala."
Damiani alionekana kupoteza hata hamu ya kuendelea na mazungumzo. Aliamini kuwa nafasi hiyo moja, iliyokuwa ikigombaniwa na mamia ya wahitimu, haingekuwa yake kabisa. Alijikatia tamaa kimoyomoyo.
Baada ya muda, wakatangaziwa kuwa matokeo yatatoka kesho. Wale waliopita watajulishwa, na wasipopokea ujumbe au simu kufikia saa nne asubuhi, basi wafahamu hawajapita.
Damiani alipoteza tumaini kabisa. Aliona kama alipoteza pesa zake bure kuja jijini Dar. Alitamani kurudi Lushoto kwao siku hiyo hiyo, lakini akajiambia asubiri kwanza. Hata hivyo, aliona kuwa chuo kikubwa si kigezo cha mafanikio—cha msingi ni kuwa na uwezo halisi (competence).
Siku iliyofuata, Damiani alikuwa na furaha sana. Alikuwa tayari amepokea ujumbe kuwa amepita kwenda kwenye oral interview! Alimshukuru Mungu na kujipanga kikamilifu kwa hatua iliyofuata.
Akiwa amejaa matumaini mapya, alielekea kwenye jengo la kampuni hiyo. Wakati huo huo, gari aina ya Audi New Model, rangi nyeupe, lilisimama. Alishuka Merina, ambaye alionekana kuendesha yeye mwenyewe.
"Mambo!"
"Poa, za toka jana?"
"Safi! Hongera."
Comments