Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

Baada ya Damiani kumaliza mahojiano ya kazi, alitoka akiwa amepewa maelekezo kwamba majibu yatatolewa ndani ya siku kumi zijazo, ikibainika kama amepata kazi au la.

Aliondoka moja kwa moja kutoka eneo hilo na kupanga kusafiri kuelekea Tanga siku hiyo hiyo, kwani muda ulikuwa unaruhusu. Saa sita kamili alikuwa ndani ya basi la Mining Nice akielekea Lushoto. Alikuwa na nusu tumaini la kupata ajira, kwani ingawa alijibu maswali vizuri, bado alihisi kushindwa na yule msichana aliyekuwa kwenye usaili naye. Kila alipomkumbuka, alihisi kwamba kumshinda mtu aliyesoma katika moja ya vyuo vikubwa duniani lilikuwa jambo gumu. Alijua kuwa mfumo wa Tanzania mara nyingi huangalia chuo mtu alichosoma, hali iliyomfanya asihisi uhakika wa nafasi yake.

Saa moja kamili usiku, aliwasili Lushoto mjini, akashuka na kuelekea moja ya magari madogo (Noah) yaliyokuwa yakielekea kijijini kwao. Kwa bahati nzuri, alikuta gari lililokuwa linakaribia kujaa, akapanda na kusubiri abiria wengine. Hatimaye, waliondoka kuelekea kijijini kwao, Mkuzi.

Japokuwa alikuwa na mawazo mengi, mara kwa mara picha ya yule msichana ilimjia akilini. Aliwaza kwamba kama rafiki yake Elvis, ambaye alipenda sana wanawake wazuri, angekuwa kwenye nafasi yake, asingejali sana usaili huo bali angeweka juhudi zaidi katika kumtongoza yule mwanamke. Alipomkumbuka, alijikuta akitabasamu na kukiri kuwa msichana huyo alikuwa mrembo sana, pengine hata nje ya uwezo wake wa kumfikia.

Akiwa bado kwenye mawazo, alishtushwa na kondakta aliyemjulisha kuwa amefika Mkuzi. Alitazama nje kuthibitisha mahali alipokuwa, akaona kuwa kituo chake cha kushukia kilikuwa mbele kidogo. Alimjulisha kondakta kuhusu hilo, na alipofika eneo husika, alishuka na kuanza kushuka kwenye kijimlima kuelekea kijijini kwao.

Kijiji cha Mkuzi kilikuwa kimeendelea; umeme ulikuwa umesambaa kila kona, na kulikuwa na harakati nyingi za watu. Mara tu baada ya kushuka, baadhi ya wakazi waliomfahamu walimsalimia, na watoto walikimbia kumchukua mizigo yake na kupeleka nyumbani.

Maombolezo ya Taifa

Ilikuwa ni siku chache tangu Rais wa Tanzania afariki dunia, na taifa lilikuwa bado kwenye maombolezo ya siku ishirini na moja. Japokuwa kiongozi huyo tayari alikuwa amezikwa, Watanzania wengi waliompenda bado walimhuzunikia kwa sababu ya jinsi alivyokuwa kipenzi cha watu.

Naam! Bendera Onyango alikuwa Rais wa awamu ya nane wa Tanzania. Alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa na msimamo thabiti katika utawala wake, hali iliyomfanya apendwe sana na kundi kubwa la Watanzania, huku pia kundi lingine likiwa halimpendi – jambo la kawaida katika siasa. Pamoja na hayo, licha ya kutokupendwa na baadhi ya watu, Rais Onyango alijitahidi sana kutekeleza majukumu yake, hususan yale aliyoyaahidi wakati wa kampeni zake. Alikuwa na makamu wake, Bwana Henri Mushi, ambaye alisimama naye bega kwa bega katika utawala wake.

Kwa kiasi kikubwa, Bendera Onyango alifanikiwa kutimiza ahadi zake, hususan katika sekta ya miundombinu. Msimamo wake mkali kuhusu usimamizi wa kodi ulimletea wafuasi wengi. Hata hivyo, baadhi ya watu hawakumkubali, iwe kwa sababu za msingi au zisizo na msingi, kwani hakuna binadamu aliye mkamilifu. Vivyo hivyo, hata Rais Bendera alikuwa na mapungufu yake kama kiongozi.

Moja ya mafanikio makubwa ya utawala wake lilikuwa ni kukomesha biashara ya madawa ya kulevya nchini. Kwa kushirikiana na wasaidizi wake na Jeshi la Polisi, alihakikisha anaziba mianya yote ya uingizwaji na usafirishaji wa dawa hizo. Kwa kiwango kikubwa, alifanikiwa, lakini mafanikio hayo pia yalimletea maadui wengi, hususan kutoka kwa wafanyabiashara wa madawa hayo.

Hata hivyo, hakufanikisha hayo peke yake. Alifanya kazi kwa karibu na mawaziri wake, na kwa bahati mbaya, baadhi yao walikuwa washirika wa biashara hiyo haramu. Mmoja wa wafanyabiashara hao alikuwa Bwana Bruno Lamberk, mzungu aliyekuwa ameishi Tanzania kwa zaidi ya miaka ishirini. Alikuwa mwekezaji mkongwe nchini na mmoja wa matajiri wakubwa, lakini mbali na biashara zake halali, alikuwa pia kinara wa biashara ya madawa ya kulevya katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Haikujulikana wazi kama Bruno Lamberk alikuwa na familia au la, kwani hakuwahi kuonekana akiishi na mwanamke yeyote, isipokuwa wale  wanawake walikuwa wakija kufanya starehe na kuondoka. Basi, bwana huyu, mara baada ya Rais Bendera kuingia madarakani, haikujulikana alitumia mbinu gani kumnasa hadi ikapelekea bwana Bruno kutoa ushirikiano na kuwasaliti wauza madawa wenzake. Hatimaye, biashara hiyo ilifungiwa kabisa nchini Tanzania, na wauza madawa maarufu walikimbilia nje ya nchi.

Mmoja wa waliokimbilia nje ya nchi alikuwa bwana Samuel Saitoto (Rich Sam), muuza madawa mkubwa ndani ya mtandao wa bwana Bruno. Baada ya kusalitiwa na rafiki yake, aliamua kukimbilia Mexico pamoja na familia yake.

Habari ya kifo cha Rais Bendera ilikuwa pigo kubwa kwa Bruno, kwani Rais huyo ndiye aliyekuwa akimpa ulinzi mkubwa dhidi ya maadui zake. Sasa ni siku ya ishirini tangu kuzikwa kwa Rais Bendera nchini Tanzania. Bruno alikuwa amejificha ndani ya jiji la Tanga, wilayani Lushoto.

"Mkuu, nimefanikiwa kuongea naye. Anaonekana ni kijana shupavu. Akipewa mafunzo maalumu, atafaa kabisa," alisema mwanaume mmoja aliyekutana na Damiani ndani ya jiji la Dar es Salaam. Wawili hao walikuwa na mazungumzo mazito kuhusu jambo fulani.

"Good! Nimempenda yule kijana, na piga ua, piga chini, lazima tumuingize kwenye system. Endelea kumfuatilia, maana muda si mrefu tuta-execute the plan. My enemies are looking for me. Bendera is dead. No one can protect me now," alisema kwa msisitizo, akimaanisha kuwa muda mfupi ujao mpango wao utaanza kutekelezwa.

"Inabidi uondoke nchini hii."
"Siwezi, Danny. Nitafia hapa hapa Tanzania."
"But it’s too dangerous!" (Lakini ni hatari sana!)
"Najua, na ndiyo maana nakwambia endelea kum-track Damiani. We need to prepare him." (Akiwa na maana kwamba wanatakiwa kumuandaa mapema.)

Mpango wa Kumbomoa Bruno

Kimbona, kama alivyoahidiana na Samu juu ya kumtafuta Bruno na kumuangamiza, hakutaka mpango huo kufeli. Kila alipokumbuka kiasi cha pesa alichopoteza baada ya Bruno Lamberk kuwasaliti, hasira zake ziliongezeka. Alikuwa na kila sababu ya kuhakikisha Bruno anatoweka kabisa.

Kwa muda mrefu, Kimbona alikuwa amepumzika katika biashara hiyo, lakini watu wake wa mtandao (gang) bado walikuwepo nchini, akiwalipa kwa siri kwa ajili ya siku atakaporudi tena kwenye mchezo. Kifo cha ghafla cha Rais Bendera kilionekana kama fursa ya dhahabu kwake kurudi kwa kishindo katika biashara ya madawa ya kulevya.

"Derick, hakikisha unawapanga vijana mkao wa kazi. Taarifa kutoka kwa shushu wetu ndani ya TISS zinasema kuwa Bruno kajificha wilayani Lushoto, kwenye Mambo View Hotel."

"Sawa mkuu, vijana wako tayari, wanasubiri tu maelekezo yako."

"Basi safi. Pumzika kwa leo. Kesho nitakupa maagizo kamili. Hakikisha hili jambo linashughulikiwa kwa weledi wa hali ya juu. Hakuna kufeli!"

"Sawa boss."

Baada ya mazungumzo hayo, Kimbona alicheka kwa dharau huku akigugumia wine yake aina ya Black & White.

"Hahahaha… hahaha… hii ni fursa nyingine kabisa kwangu! Ninaenda kurudi ulingoni muda si mrefu. Bruno… Bruno… ama zako, ama zangu!"

******

Siku iliyofuata, Derick alipokea simu kutoka kwa bosi wake, akimtaka afike kwenye kampuni yake iliyopo katika jengo la LAPF Tower. Kampuni hiyo ilijulikana kwa jina la KILAC (Kimbona International Link and Companies).

Derick hakupoteza muda. Alipofika ofisini, alipokewa na secretary kisha akarudishwa moja kwa moja kwa bosi wake. Baada ya salamu, alipewa ramani kamili ya mpango wao.

"Kuwa makini na Danny. Huyu ni jasusi wa kimataifa, ana mbinu nyingi za kuwazidi. Lakini na ninyi pia mna mbinu za kumzidi akili. Narudia tena, hili suala halina kufeli! Hakikisheni mnalimaliza ndani ya siku kumi zijazo."

"Sawa boss."

Baada ya mkutano huo, Derick hakutaka kupoteza muda. Aliitisha kikao cha dharura na genge lake la kimafia, kisha wakapanga safari ya kuelekea Lushoto.

*******

Damiani na Shauku ya Ajira

Siku kumi zilipita bila Damiani kupokea ujumbe wowote kutoka kwa kampuni aliyofanyia usaili. Mama yake alimtia moyo asikate tamaa, lakini kwa upande wake, hakujiona na nafasi yoyote ya kupata kazi hiyo.

Alimwangalia mama yake, aliyekuwa amevaa nguo zilizochanika na zisizovutia. Alimuonea huruma. Alitamani kumtoa mama yake kwenye lindi la umasikini kwa kadri ya uwezo wake. Alimpenda sana mama yake, kwani alijua jinsi alivyohangaika kuhakikisha anasoma.

Aliwalaumu viongozi wa serikali kwa kushindwa kutengeneza mfumo mzuri wa ajira kwa wahitimu. Wazazi walihangaika kuwasomesha watoto wao kwa gharama kubwa, lakini walipomaliza, ajira hazikuwepo.

Siku hiyo, Damiani alibaki nyumbani kumsaidia mama yake. Alikuwa akitengeneza banda lao la mbuzi uwani, lakini kila mara alikuwa akiangalia simu yake kwa matumaini ya kupokea ujumbe. Saa zilipita—hakuna simu, hakuna ujumbe.

Hatimaye, aliamua kutoka kwenda shambani kwao kuchukua miti ya kumalizia banda la mbuzi. Alichukua mwendo wa nusu saa kupita kijijini kwao. Siku hiyo kulikuwa na sherehe kanisani, na wengi walikuwa barabarani.

Baada ya dakika arobaini na tano, aliingia kwenye shamba lao kubwa la miti ya biashara. Hakutaka kupoteza muda, alianza kukata mikalitusi iliyo nyooka.

Wakati akiendelea, simu yake ilitoa mlio wa ujumbe. Akaendelea kukata miti hadi aliporidhika na idadi aliyokusanya, ndipo akatoa simu yake kuangalia.

"HONGERA BWANA DAMIANI RABANI! UMEFANIKIWA KUPITA KWENYE INTERVIEW. UNAPASWA KURIPOTI KAZINI MAPEMA KABLA YA TAREHE HII."

Machozi ya furaha yalimtiririka. Alijikuta anaruka kwa shangwe. Hakumalizia kazi, badala yake alikimbilia nyumbani kumweleza mama yake habari njema.

Lakini wakati anarudi, alisikia kishindo kizito upande wake wa kushoto.

Aligeuka haraka—

Lahaula!

Mtu mmoja mwenye ngozi nyeupe alikuwa ameanguka, huku akivuja damu nyingi usoni na ubavuni!

Damiani alipatwa na woga. Akili yake ilimwambia KIMBIA!

USIKOSE SEHEMU IJAYO

Previoua