CHANGE
Story by Elton Tonny
Urafiki, Familia, Mapenzi, Mahaba, Tamaa, Hila, Usaliti, Unyanyasaji, Ukatili, Mauaji, Mambo yasiyotazamiwa, Mambo yenye kuhofisha
R-rated 18+
★★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA SABA
★★★★★★★★★★★★★★
Mwanasheria? Mwanaume huyo kijana mwenye sura nzuri, mwili imara wa kuvutia mwanamke yeyote yule, na pigo za kibabe kama siyo usharobaro, Draxton alikuwa ni mwanasheria? Blandina akamtazama Namouih machoni kwa njia ya mshangao, naye Namouih akamwangalia rafiki yake kwa ufupi kisha akamkazia macho mwanaume huyo.
"Kulikuwa na jam kidogo mheshimiwa... samahani sana kwa kuchelewa..."
Mwanaume huyo akasema hayo, akionekana nadhifu zaidi tofauti na jinsi alivyoonekana mara ya kwanza alipokutana na marafiki hawa wawili siku ile.
"Wewe ndiyo mwanasheria wake Japheth Warioba?" hakimu akamuuliza.
"Ndiyo, mimi ni mwanasheria wak...."
Mwanaume huyu alikuwa amefikia mbele zaidi, kwenye kimlango kidogo kilichopatenganiaha kule mbele na sehemu za mabenchi huku nyuma, naye akaishia hapo na kusimama kwanza. Namouih alimwangalia na kuona anainamisha uso wake kidogo kama vile anavuta hisia fulani hivi, halafu akageukia upande aliokaa Namouih na kumtazama machoni moja kwa moja. Alimwangalia Namouih kwa macho fulani hivi kama ya udadisi, ukali, yaani kama vile mtu anayejiuliza "huyu anafanya nini hapa," naye Namouih akamshusha na kumpandisha kisha akatazama mbele kwa njia iliyoonyesha hakumjali.
"Ningependa kuona utambulisho wako tafadhali," hakimu akasema hivyo.
Mwanaume huyu akaacha kumwangalia Namouih na kusema, "Bila shaka," kisha akavuka kimlango cha hapo na kwenda kumpa msomaji utambulisho wake yeye kama mwanasheria, halafu akasimama pembeni yake Japheth. Namouih alikuwa anamwangalia sana, hata Blandina alipigwa na butwaa kwa kweli, yaani hakutegemea.
Hakimu alipoona uthibitisho wa utambulisho wa mwanasheria huyo, akatamka kwa sauti, "Maximilian Draxton."
Hilo ndiyo lilikuwa jina lake. Draxton akatikisa kichwa kukubali, kisha hakimu akamrudishia msomaji utambulisho huo naye akaupeleka kwa mwanasheria huyo wa Japheth. Akaulizwa kwa nini hakuwa amevaa joho la mwanasheria, naye Draxton akamwambia hakimu kwamba lilisahaulika tu kwa sababu ya haraka yake kuja huku. Hivyo akatendewa tu kwa fadhili na mahakama kwa kupewa vazi kama hilo la ziada, kwa sababu ndiyo jinsi utaratibu wa mahakama ulivyokuwa; lazima kuvaa joho.
Mwanasheria huyu akalivaa hapo hapo na kuketi pembeni yake Japheth, na kijana huyu alionekana kutulia zaidi baada ya ujio huu wa Draxton. Sasa kulikuwa na hali ya utulivu zaidi, naye hakimu akaruhusu majibizano ya kesi a.k.a trial, yaanze. Taratibu hii huanza rasmi kwa mwanasheria wa mtoa mashtaka kutakiwa kutoa utangulizi wa mwanzo kuhusu mambo hakika ya kesi hiyo. Namouih akasimama na kuanza kuelezea jinsi kisa cha Agnes kilivyokuwa.
Binti huyu aliitwa Agnes Mhina, umri miaka 19, na alikuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na kijana aliyekwenda kwa jina la Japheth Warioba mwenye miaka 26. Mapenzi yao yalidumu kwa miezi isiyopungua 16, yaani karibia mwaka mmoja na nusu, na baada ya hapo, kama Agnes anavyodai, kukatokea hali ya kutoelewana baina yao, na hivyo binti huyo akaamua kuachana naye. Lakini huyo kijana wa kiume hakulichukulia suala hilo kirahisi, na kwa sababu ya ubinafsi akamlazimisha binti huyo kufanya mapenzi kwa njia yenye jeuri kubwa sana iliyomuumiza msichana. Huu ulikuwa ni ubakaji haijalishi hali ya uhusiano waliokuwa nao kabla, kwa sababu Agnes aliingiwa kinguvu na mwanaume huyo kijana bila ya yeye kutaka. Ushahidi wao wenye nguvu zaidi ulikuwa ni karatasi za vipimo kutoka kwa daktari zilizoonyesha kwamba kweli Agnes alibakwa, lakini pia kulikuwa na video kutoka kwenye kamera iliyotegeshwa ambayo ilichukua tukio hilo; sauti za Agnes na Japheth zikisikika vyema ndani yake.
Baada ya kuelezea hayo, Namouih akaketi, kisha hakimu akamuuliza mwanasheria wa mtuhumiwa kama naye pia alitaka kutoa utangulizi kwa upande wake, lakini Draxton akakanusha. Hii ilimfanya Namouih acheke kimoyomoyo kwa sababu aliona ni kama jamaa alikuwa hajui anachokifanya, kwa hiyo hakimu sasa akasema ulikuwa muda wa kuita mashahidi. Upande wa mtoa mashtaka, yaani Agnes, kulikuwa na mashahidi wanne tu ambao walitosha kabisa; mama yake Agnes, askari aliyemkamata Japheth, rafiki wa karibu wa Agnes aliyeitwa Mamu, na daktari aliyefanya vipimo vya Agnes. Upande wa mtuhumiwa Japheth haukuwa na shahidi hata mmoja, kwa hiyo ingetakiwa baada ya Namouih kuwahoji mashahidi wake, Draxton awahoji pia.
Mmoja baada ya mwingine wakaitwa na Namouih, naye akawauliza maswali mengi vizuri na kwa njia ambazo zilitokeza majibu yaliyoonyesha kwamba kweli janga lile lilimkuta Agnes. Mama yake alidai kwamba siku hiyo Agnes hakurudi nyumbani kabisa. Askari aliyemkamata Japheth siku tatu baada ya tukio akasema alimshika Japheth akiwa nyumbani kwao. Mamu akasema siku ambayo Agnes alibakwa, rafiki yake huyo alikwenda "getoni" kwake na kulala, na alimsaidia kupunguza maumivu sehemu zake za siri kabla ya kwenda kwa daktari. Daktari akasema kwamba kweli kama majibu yalivyoonyesha, binti alichubuka sana sehemu za siri, na hiyo ingesababisha vidonda, akikazia kuwa bila shaka Japheth alitumia jeuri ya kinyama.
Blandina alikuwa anamwangalia Draxton. Jinsi mwanaume huyo alivyokuwa ameweka umakini wake wote kule mbele, yaani ilikuwa kwa njia kuu sana, iliyomwambia kwamba hapo alikuwa na jambo lake muhimu. Baada ya Namouih kumaliza kuwahoji mashahidi wake, akarudi kukaa akiwa amewaambia waamuzi kwamba kutokana na hayo yaliyosemwa ni wazi kabisa kwamba upande wake ndiyo uliokuwa "mwathirika."
Sasa ikawa zamu ya mwanasheria wa mtuhumiwa kuwahoji mashahidi wale wale wa upande wa mtoa mashtaka. Draxton akanyanyuka na kwenda hapo mbele, na kila mtu alitulia sana ili waweze kuona kama angeweza kuweka mambo kuendana na njia ya Namouih ya kuzungumza bila hofu yoyote. Namouih na Blandina walikuwa wanamtazama kwa umakini pia.
Akaanza kumhoji mama yake Agnes, kisha akafata Mamu. Alikuwa na njia fulani hivi ya taratibu ya kuzungumza, iliyofanya aonekane kuwa mtu makini lakini aliyejua sana kucheza na akili. Aliuliza maswali kwa njia ambazo mwanzoni yangeonekana kutokuwa muhimu kabisa, lakini mwishoni angeyarudia kwa njia tofauti iliyowakosoa mashahidi hao na kuwaacha wakiwa wamechanganyikiwa. Mama ya Agnes na Mamu, wote walifika hatua ambayo hawakuweza kuendelea kuongea kutokana na kushindwa wajibu nini, na Draxton akawaruhusu tu warudi kukaa. Askari aliyemkamata Japheth aliongea kwa njia nzuri na ya uwazi kabisa kwa kujibu maswali yote bila kuchanganya mambo, naye akarudi kukaa pia.
Kisha sasa akaingia daktari wa Agnes. Draxton akauliza majina yake, amesoma wapi, alifanyia kazi wapi, na ikiwa aliamini kwamba umri wa Agnes ulimruhusu kuwa na mahusiano. Akaanza kuulizia wakati ambao vipimo hivyo vilichukuliwa, na ikiwa ni kweli kwamba binti alikuwa na michubuko basi ingesababisha vidonda ambavyo mpaka kufikia wakati huu bado vingekuwepo, na kwa kuwa ripoti hiyo ya vipimo ilitoka kwenye maabara yake binafsi, Draxton akapendekeza wachukue vipimo kwa mara nyingine tena, na wakati huu iwe ni kwa misingi ya mahakama ndani ya hospitali kubwa kabisa na siyo kwa hiyo ripoti kutoka maabara ambayo ilikuwa imeshatengenezwa tu haraka.
Namouih alipinga vikali hoja zake, akisema huo wote ungekuwa ni usumbufu kwa kuwa mbali na majibu ya vipimo hayo kuja yakionyesha ni kweli Agnes alibakwa, kulikuwa na ushahidi wa ile video ambayo ndiyo ilikuwa inakata maneno yote hapo. Daktari alikuwa amebaki kimya tu, hivyo Draxton akamwambia akakae Ili ashughulikie suala la video hiyo kwa kumhoji mtoa mashtaka mwenyewe, yaani Agnes. Hali ndani hapo ilikuwa imeanza kuwa rusha roho, kwa kuwa ilianza kuonekana kwamba Draxton anataka kufichua jambo fulani zito sana, lakini kila mtu alitaka kuona haya yote yangeishia wapi.
Mwathiriwa akapanda kizimbani hatimaye, na alikuwa binti mmoja ambaye kwa kumtazama tu ungesema ana nyodo sana, ila kwa hapo alikuwa anaonyesha unyonge wa hali ya juu. Draxton akamkaribia na kumpa tabasamu hafifu, huku Agnes akimtazama kwa njia fulani hivi ya kujihami.
"Mambo?"
Draxton akatoa salamu hiyo kumwelekea Agnes, kwa njia ya kirafiki kabisa. Namouih alikuwa ameshakerwa naye sana kufikia hapo ila basi tu, hakuwa na jinsi. Baada ya Draxton kuanzisha maswali kuhusu utambulisho wake Agnes, shule, kama alifanya kazi, muda aliokuwa kwenye uhusiano na Japheth, hata mara ambazo alifanya naye mapenzi, sababu ya kutoelewana kwao, na mambo mengine, akafikia swali hili:
"Ulimwambia nani kwanza baada ya jambo unalosema lilikupata kukupata?"
"Mamu..."
"Oh, siyo mama, ni Mamu?"
"Ndiyo..."
"Baada ya hapo ndiyo mkaenda kwa askari?"
"Ndiyo..."
"Na mkaulizwa maswali mengi kuhusiana na yaliyotokea?"
"Ndiyo..."
"Majibu yako yote kwa wakati huo yanafanana kabisa na kisa chote kilivyotokea usiku unaosemwa uliingiwa vibaya kimwili?"
"Napinga kauli mheshimiwa. Anauliza vitu visivyokuwa na uendani wowote kwenye ushahidi uliotolewa," Namouih akamwambia hakimu.
"Pingamizi limekataliwa," hakimu akasema.
Namouih akakaa na kuangalia pembeni kwa kukerwa.
"Unafikiri kwamba ikiwa uchunguzi ungefanywa kwa wakati huu kwa mara nyingine tena, kila kitu kinachodaiwa kuwa kimeshatokea kitaonekana kuwa ni kweli au uwongo?" Draxton akauliza.
Agnes akabaki kimya.
"Unajua utofauti uliopo kati ya kile ambacho watu wataamini kwa kuwa ni ukweli, na kile ambacho wanaamini kwa sababu wanafikiri wanaujua ukweli?"
"Napinga kauli mheshimiwa, ni mambo yasiyopatana na ushahidi," Namouih akaingilia kati.
"Pingamizi limekubaliwa," hakimu akasema.
Draxton akaendelea kumchimba Agnes....
"Okay, kwa hiyo ulisema kwamba siku hiyo mlikuwa wapi... motel... au lodge?"
"Lodge..."
"Jina la hiyo lodge?"
Agnes akabaki kimya.
"Haujui jina la hiyo lodge? Unalijua? Hulikumnuki? Unalikumbuka?"
"Napinga kauli mheshimiwa, anauliza maswali na kujijibu mwenyewe," Namouih akasema.
"Pingamizi limekataliwa..." hakimu akasema.
Draxton akaendelea...
"Mlikuwa na kawaida ya kukutana kwenye lodge eh?"
"Hapana..."
"Ilikuwa kwa siku hiyo tu?"
"Ndiyo..."
"Unajua kuwa kuitana mpaka kufika lodge inamaanisha kwamba ulikwenda kwa kupenda, siyo kwa kulazimishwa, endapo kama tayari mlikuwa mmeshaachana kwa kutoelewana?"
"Napinga kauli mheshimiwa...."
"Pingamizi limekataliwa. Maximilian endelea," hakimu akamkatisha Namouih.
"Elezea ilivyokuwa mpaka ukakubali kukutana naye lodge siku hiyo..."
"Ali... alinipigia simu, akaniomba sana tukutane kwa sababu alisema anataka kuniomba msamaha, ndiyo nikaenda halafu akanifanyia hivyo," Agnes akasema.
"Mwongo! We' ni mwongo!" Japheth akapayuka kwa sauti ya juu, naye akaambiwa atulie na kuiheshimu mahakama.
"Okay, kwa hiyo ukaenda lodge. Bila shaka lodge huwa zina watu ndani... na mtu wa mapokezi. Kwenye maelezo yako kwa askari ulisema Japheth alikulala kinguvu kwa muda usiopungua dakika 20 kufikia 30. Lodge hapo. Hakuna yeyote aliyesikia labda unapiga kelele au..."
"Aliniziba mdomo," Agnes akaongea upesi.
Namouih akakaza macho kwa mshangao. Hii ilikuwa kwa sababu fulani ambayo aliitambua haraka, na Draxton angeifunua muda siyo mrefu.
"Alikuziba mdomo. Kwa hiyo hakuna sauti yoyote iliyosikika, si ndiyo? Hamna mtu ambaye angeweza kuja kukusaidia eeh?"
Agnes akatikisa kichwa kukubali, bila kuelewa kwamba alikuwa amejikanyaga.
"Okay, sasa ndiyo tutaingia kwenye suala la video. Kwa hiyo... video iliyochukuliwa ilitokana na kifaa gani?" Draxton akauliza.
"Simu..."
"Simu ya nani?"
"Yangu."
"Uliitegesha wakati gani?"
"Nilipofika hapo."
"Hapo Lodge? Aah... kumaanisha wa kwanza kufika ilikuwa wewe? Kwa hiyo aliyelipia chumba ni wewe?"
"Alilipia yeye... angelipa baadaye..."
"Lodge... okay. Kwa hiyo ukaitegesha camera, halafu ndiyo akaja, toka amefika camera tayari ilikuwa inarekodi kila kitu, si ndiyo? Ulikuwa umeitegesha tu ili lolote ambalo lingetokea ije kuthibitika baadaye kwamba kweli lilitokea?"
"Pingamizi mheshimiwa, anauliza na kujijibu," Namouih akasema.
"Pingamizi limekubaliwa..." hakimu akasema.
"Okay. Kwa hiyo maongezi ya kuombana msamaha yakageuka kuwa show ya ubakaji... kwa nini?" Draxton akauliza.
"Alikuwa ananilazimisha me nikakataa... nikamwambia nataka kwenda nyumbani, mimi na yeye basi... lakini akanilazimisha... akanivuta kitandani akani... akanivua..."
Japheth alikuwa anatikisa kichwa huku akimtazama Agnes kwa njia iliyoonyesha hasira sana.
"Ilikuwa ni siku ya shule au weekend?" Draxton akamuuliza Agnes.
"Ilikuwa... ilikuwa siku ya shule... juma ngapi sijui..."
"Ulimuaga mama unaenda wapi?"
"Kwa rafiki yangu."
"Ilikuwa saa ngapi?"
Agnes akabaki kimya.
"Saa tatu? Saa nne? Usiku wa manane?"
"Pingamizi mheshimiwa, anauliza na kujibu..."
"Pingamizi limekataliwa..." hakimu akamkatisha tena Namouih.
Draxton akauliza, "Kwa hiyo, alipoanza kukugusa na kukuvuta kitandani, hukupiga kelele?"
"Nimekwambia aliniziba mdomo," Agnes akajibu kwa kukerwa.
Namouih akainamisha uso wake na kutikisa kichwa kwa kusikitika.
"Okay, hapo hapo, kwa mara nyingine tena, unasema alikuziba mdomo, si ndiyo? Sauti zinazosikika kwenye video uliyorekodi zilitoka wapi?" Draxton akauliza.
Agnes akabaki kinywa wazi na kushindwa kutoa jibu.
"Ni wewe mwenyewe ndiye uliyefika kwenye lodge, ukategesha simu yako kwa camera, si ndiyo?"
Kimya.
"Ulipanga hii yote Agnes, siyo?"
Kimya.
"Kwa hiyo Japhet alipofika, mkayajenga, au mkayavuruga? Kwenye video inaonyesha ukiwa tupu kabisa huku chini, alifika mkagombana tena lakini akawa na muda wa kukuvua nguo huku amekuziba mdomo? Ulivaa gauni tu usiku huo? Hukuvaa nguo yoyote ya ndani?"
"Pingamizi mheshimiwa..."
"Limekataliwa..."
"Ulivaa nguo ya ndani? Hukuvaa?"
"Nilivaa!" Agnes akasema huku machozi yakianza kumtoka.
"Oh, kwa hiyo tukiiangalia video tena tutaona nguo yako ya ndani inaondolewa, si ndiyo?"
Kimya.
"Mara ya mwisho umeangalja hiyo video ilikuwa lini Agnes? Hautakiwi kusikika ukilia kama ilivyo kwenye video kwa kuwa alikuziba mdomo wako, si ndiyo? Hizo sauti kwenye video ni kutokea wapi sasa? Haupigani naye kabisa, miguu iko juu vizuri tu, si ndiyo? Ulimfungulia miguu yako we' mwenyewe si ndiyo? Ndiyo kilichotokea usiku huo, lakini sasa hivi tuna mambo mengine kabisa, siyo? Majibu ya vipimo yalikuwa yako au ya nani sasa? Ikiwa siyo yako daktari ameyatoa wapi...?"
Agnes akatazama upande wa mabenchi kule nyuma.
"Kwa nini umemwangalia daktari?" Draxton akamuuliza, bila yeye kuwa amegeuka nyuma.
Agnes akamwangalia huku pumzi zake zikiongezeka kasi.
"Unaweza kuwaambia waamuzi sababu inayokufanya ushindwe kutoa majibu? Ni kwamba hukumbuki vizuri kilichotokea au? Unakumbuka? Haukumbuki? Unakumbuka lakini ni kwamba haujui?"
Agnes akiwa kama shahidi mkuu hapa akashindwa kutoa majibu na kuendelea tu kulia.
Draxton akaendelea kuuliza, "Unakumbuka kwamba umetoa kiapo cha kusema ukweli tu, na ukweli mtupu? Unajua ni nini kitakupata ikigundulika umedanganya chini ya kiapo?"
"Pingamizi mheshimiwa... anamsukuma shahidi kupita kiasi," Namouih akaingilia kati.
Hakimu akatulia kidogo, kisha akasema, "Pingamizi limekubaliwa."
Draxton akaendelea kuuliza maswali kama hayo bila kumpumzisha Agnes afikirie hata mara moja. Watu wote walikuwa wanaangaliana na kusikika wakinong'ona, kwa kuwa itikio la Agnes lilionyesha wazi kwamba alikuwa njia panda. Namouih akamtazama sana Agnes, akishindwa kuamini kama kweli kuna mwanamke angeweza kudanganya kuhusiana na jambo kama hilo, kwa sababu ilikuwa wazi kwa yeyote hapo kwamba binti alikuwa amedanganya. Akaendelea kulia tu akiwa kizimbani hapo, hivyo Draxton akamwambia hakimu kwamba alikuwa amemaliza maswali yake, naye angependa kutoa maoni yake ambayo alikuwa ameamua kusubiri mpaka wakati huu ili aweze kuyasema.
Akawaambia waamuzi kuwa mambo mengi kuhusiana na tuhuma za tukio hilo yalitakiwa kufanyiwa uchunguzi kwa mara nyingine tena. Sawa ushahidi walikuwa nao, lakini alitaka wahakikishe kabisa kwamba ushahidi huo uliokuwa halali vinginevyo wangejikuta wanatoa uamuzi wa kumfunga kijana asiyekuwa na hatia. Alielewa kwamba hii ndiyo iliyokuwa mara ya mwisho ya usikilizaji wa kesi hii kabla ya hukumu, lakini katika siku hizo chache mpaka kuifikia tarehe yenyewe, wangekuwa wameshapata uthibitisho wa kuaminika zaidi. Kwanza, Agnes afanyiwe vipimo kwa mara nyingine tena, na pili, video ile ichunguzwe vizuri badala ya kufikia mikataa isiyo ya kweli kwa kuwa tu "sauti zao zilisikika."
Baada ya hapo, mwanasheria Draxton akaenda kukaa kwenye kiti pembeni yake Japheth. Ilikuwa ni wonyesho mzuri sana wa stadi ya kazi, na aliifanya ionekane kuwa rahisi sana ingawa ilikuwa jambo gumu kufichua mambo kwa njia aliyotumia. Namouih akabaki kimya tu baada ya Agnes kurudi kutoka kizimbani na kukaa pembeni yake, akijiona kama mpuuzi kwa kiasi fulani, ingawa bado moyo wake haukutaka kukubali kwamba Agnes alikuwa amedanganya. Akamwambia kwa uhakika kwamba asijali sana kuhusu maneno yenye kuchanganya ya mwanasheria yule, kwamba bado upande wao ulikuwa na nguvu zaidi.
Binti huyo alikuwa amejikanyaga kweli kwenye sehemu ile ya kuzibwa mdomo, na ikawa wazi kwamba kisa hiki chote kilikuwa ni uwongo mkubwa sana, ingawa bado hukumu haikuwa imetolewa. Hakimu akamuuliza mwanasheria wa mtoa mashtaka ikiwa alitaka kuhoji mashahidi kwa mara nyingine tena, lakini Namouih akakanusha. Hivyo akawaomba wanasheria watoe kauli zao za hitimisho baada ya hayo, naye Namouih akasimama tena na kutoa maoni yake, akifuatwa na Draxton ambaye alikazia tena mambo aliyokuwa amesema.
Baada ya hapo, kundi la waamuzi 6 (jurors) likaingia kwenye chumba kingine kutoka sehemu hiyo ili wajadiliane kwa ufupi kuhusu mambo yote hayo, wakiwaacha watu wanasubiri warudi ili kujua wamefikia mkataa gani. Wakati huu, Namouih alikuwa anaongea na Agnes, akitaka kujua kwa nini ilionekana kama binti amedanganya tokea mwanzo, lakini akawa anasema hakudanganya bali mwanasheria yule mwingine alikuwa amemchanganya tu. Namouih akamwambia kama kila kitu alichosema kilikuwa kweli basi kingepatana na ushahidi uliokuwepo, kwa hiyo wangepaswa kusubiri tu.
Blandina alikuwa ameelekeza zaidi fikira zake kwa Draxton. Mwanaume huyo alikuwa ameonyesha akili nzuri sana hapo, lakini kilichokuwa akilini mwake Blandina ilikuwa kwa nini, baada ya kumpa namba zake na kuahidiwa kwamba angetafutwa, hakuwa ametafutwa. Alikuwa anatamani hata amfate hapo hapo amuulize, lakini akaamua kuvunga tu kama vile hamjui. Muda mfupi baadaye, waamuzi wale wakatoka tena baada ya kufanya mazungumzo yao, kisha hakimu akapelekewa karatasi iliyokuwa na mambo waliyotoka kuandika baada ya kufikia makubaliano.
Hakimu akasema kwamba kutokana na mambo yote hapo, uamuzi uliofikiwa ulikuwa kupitia ushahidi huo kwa uhakika zaidi wakati huu, hivyo Agnes angefanyiwa vipimo tena, na video ile ingechunguzwa vyema ili kuona uhalali wa madai yake kwa asilimia zote. Akasema taratibu hizo zingeanza leo leo, kwa hiyo hakukuwa na haja ya kuweka tarehe ya mbali sana kuja kusikiliza hukumu; kesho hiyo hiyo mida ya saa saba ndiyo hukumu ya kesi hii ingesomwa. Baada ya kusema hayo, akagonga nyundo yake ya mbao pale mezani, kisha akaondoka, na watu wakaanza kunyanyuka pia huku wakiendelea kuliongelea sana jambo hilo.
Japheth akarudishwa na askari wake mlinzi kule alikopaswa kufungiwa, huku ndugu zake wakibaki kuzungumza na mwanasheria wake. Namouih akatoka nje pia pamoja na Agnes na mama yake kuzungumza naye, kwa kuwa sasa ilionekana kweli kwa upande wa dada huyu kulikuwa na jambo lenye nuksi, na hivyo akawa anataka kujua ikiwa hakupewa taarifa za kutosha. Lakini Agnes akamhakikishia na kuendelea kumhakikishia kwamba upande wake ndiyo uliokuwa umeonewa, na akazidi kumwomba Namouih ampiganie kwa nguvu zote ili haki itendeke kweli.
Blandina alikuwa anasubiri sehemu ya mwingilio wa jengo hilo la mahakama, na aliyekuwa akisubiriwa ni Draxton. Alitaka sana kuzungumza naye hasa kuhusiana na ni kwa nini hakuwa amemtafuta kama alivyokuwa amemwahidi. Haikuchukua muda mrefu sana na watu wa familia ya Japheth wakatoka na kuondoka. Blandina akawa anasubiri kwa hamu sana mwanaume yule atoke pia, lakini akawa anakawia. Hivyo akaamua kurudi ndani na kuangalia alipokuwa, naye akamwona akiwa amesimama na mmoja wa waamuzi wale, ambaye alikuwa mwanamke wa miaka kama 40 hivi, na alionekana kuzungumza naye kwa shauku sana kuonyesha ni kama walifahamiana vizuri.
Akaendelea kumsubiri tu bila kujionyesha, na sasa mwanamke huyo akaonekana akichukua simu ya Draxton na kuandika jambo fulani hapo; makisio ya Blandina ikiwa ni namba za simu. Blandina akazungusha macho yake kwa kukerwa sana na jinsi mwanamke huyo alivyoonyesha kujitongozesha waziwazi, na ni hapa ndiyo akaanza kumwona Draxton anakuja upande wake ili aondoke bila shaka, naye akaanza kumfata pia.
Blandina alipomfikia karibu akasema, "Habari yako mheshimiwa... Maximilian Draxton?"
Draxton akatabasamu kwa mbali na kubaki amemwangalia tu.
"Lipi litafaa zaidi kukuita? Maximilian au Draxton?" Blandina akauliza.
"Draxton," mwanaume akajibu.
"Ndiyo ulikuwa unapiga sound kwa jury hapo au we' ndiyo ulikuwa unapigwa sound?" Blandina akauliza.
"Alikuwa ananisalimu kwa kuwa ni siku nyingi hajaniona," Draxton akamwambia.
"Salamu hadi kupeana na manamba, au siyo? Na mimi je? Tusingekutana leo ndiyo ningesahaulika kabisa eti?"
"Ona... najua sikukutafuta, ila ni kuwa... mambo mengi yaliingiliana..."
"Kuingiliana kumaanisha tokea mwanzo ulijua sisi tuko timu pinzani kwenye hii kesi eeh? Ndiyo maana ukaona unikwepe?"
"Si hivyo. Samahani Blandina," Draxton akasema kwa upole.
Blandina akatabasamu kidogo. "Em' niite hivyo tena," akamwambia.
Draxton akaangalia chini na kusema, "Blandina," kisha akamwangalia tena.
"Nikifikiri ungekuwa umeshasahau na jina langu," Blandina akasema.
"La. Nilikuwa tu busy kutafiti vitu vingi, muda ukanimeza," Draxton akamwambia.
Blandina akacheka kidogo na kusema, "Naonekana kama kupe sana eh? Kama niko desperate mno kutafutwa nawe yaani..."
"La."
"Usijali Draxton. Mimi haitakuwa na shida sana kwangu... ukiniambia tu kwamba hauwezi kupata muda kwa ajili ya...."
"No, si hivyo, I swear," Draxton akamkatisha huku akimsogelea karibu zaidi.
Blandina aliipenda sana hali hii kwa kuwa ilimfanya atambue kwamba mwanaume huyu alikuwa na mwelekeo wa kujali hisia za wengine.
"Ona, sitaki uhisi vibaya... na sikuwa na nia ya kukuacha kwenye mataa..."
"Lakini ukafanya hivyo..."
"Am sorry. Niambie ungependa nifanye nini ili kutoa kama... apology," Draxton akamwambia.
"Ni rahisi sana kwenu kusema maneno kama hayo, ila kuyatimiza sasa..."
"No, niambie. Chochote kile ambacho kitakuwa ndani ya uwezo wangu, nitafanya."
"Kweli?"
"Usiniombe gari lakini..."
"Ahahahaa... okay. Nataka unipeleke out."
"Sawa. Ungependa twende wapi? Au... me ndiyo nichague sehemu?"
"No, mimi ndiyo nachagua..."
Draxton akatabasamu kwa mbali.
"Nina wazo zuri la sehemu ya kwenda. Utatakiwa unipitie mida ya jioni ili twende huko, nataka uwe kama..."
"Date wako?" Draxton akamalizia maneno ya Blandina.
"Nilikuwa sijafikiria huko ila, inasikika vizuri," Blandina akasema.
"Sawa. Tutachekiana baadaye," Draxton akasema.
Blandina akacheka kwa chini huku akitikisa kichwa kuonyesha haamini.
"Vipi?" Draxton akauliza.
"Nahisi ni kama nitapaswa kujiandaa kwenda mwenyewe tu," Blandina akamwambia.
"La, tutaenda pamoja. Niamini," Draxton akasema kwa umakini.
Blandina akabaki kumtazama sana machoni, kama vile anauona uthibitisho wa asilimia mia moja kwamba maneno ya mwanaume huyo yalikuwa ya kweli kabisa kupitia utizami wake.
"Umeniamini?" Draxton akaongea.
"Nitaamini zaidi ukifika kweli. Lakini, utajua vipi niko wapi?" Blandina akauliza.
"Kuna app fulani ya kujua maeneo ninayo... naangalia namba yako ya simu ilipo then nakufikia. Kwa hiyo... usizime simu," Draxton akamwambia.
Blandina akatabasamu kwa njia fulani hivi kuonyesha hisia nzuri kutokana na kupenda namna mwanaume huyo alivyoongea.
"Nitakupigia. Mida ya jioni, sawa?" Draxton akasema.
Blandina akatikisa kichwa kukubali, naye Draxton akampita na kuondoka.
Mwanamke huyu alibaki hapo akimtafakari kiasi. Kuna upande fulani kumhusu Draxton uliomvutia sana, na hali ya kiutu aliyokuwa nayo ilimfanya Blandina atamani sana kujiingiza kwenye maisha yake, kwa sababu ya hali fulani isiyoelezeka alimwona kuwa tofauti na wanaume wengine aliowafahamu. Akatoka hapo pia na kuelekea nje, na sasa Namouih alikuwa amesimama pembezoni mwa gari lake, akionekana kumsubiri. Blandina akamfata huku akitabasamu kwa shauku kubwa, na Namouih akimwangalia kwa njia ya kawaida.
"Ulikuwa unaongea na huyo mtu wako bila shaka..." Namouih akasema.
"Hahah... girl mbona umekaza sana? Kafika na bonge la style yaani. Sekunde chache tu utashtukia kakuvurugia kesi haahahah..." Blandina akasema huku akicheka.
"Hawezi kufika popote na tumaneno twake twa kuwapagawisha vichwa mbovu kama wewe... alimchanganya mtoto kidogo tu, lakini haitakuwa na tatizo," Namouih akamwambia.
Blandina akacheka sana.
"Hearing ya sentence tunamaliza hii kitu kwa ushindi, na itanipa furaha kujua haushobokei mtu aliye timu pinzani," Namouih akasema.
"Ahahahah... baby tulia. Hizi kesi ni kazi tu, zitapita. Ila me Draxton simwachi salama. Anaonekana mzuri kwa bed huyo!" Blandina akaongea kwa madoido.
"We' ndiyo unayewaza kutomwacha ila yeye ashakuacha. Utaishia kuonana naye mshakamani tu kwingine ni ndoto," Namouih akasema huku akianza kuufungua mlango wa gari lake.
"Aa wapi. Leo tunakula naye," Blandina akasema.
Namouih akakunja uso kimaswali na kuuliza, "Unamaanisha nini?"
"Nimemwalika kwa ajili ya dinner leo," Blandina akasema huku akitabasamu.
Namouih akaufunga tena mlango wa gari. "What? Yaani... unataka aje leo... nyumbani?" akauliza.
"Yeah," Blandina akasema.
"Blandina... unawezaje kumwalika tu mtu ambaye hata haumfahamu... aje nyumbani... kweli hivi..."
"Si ndiyo nataka tujuane sasa? Kaniahidi atakuja..."
"Ya kukutext hakukuahidi kwani?"
"Kwani una tatizo na hilo? Ikiwa hautaki nije naye haina kwere, nitaenda naye sehemu nyingine..."
"No Blandina, sijamaanisha hivyo. Ninataka tu uwe mwangalifu..." Namouih akasema kwa upole.
"Acha basi nawe! Guy ni attorney huyo! Unajua tokea mwanzo nilidhani labda nilipagawa bure lakini sa'hivi nimejua kweli... ni Mungu ndiye alinikutanisha naye. Hadi profession zetu zinafanana! Hii haikuwa random baby, huyu jamaa napita naye," Blandina akaongea kwa uhakika.
Namouih akatabasamu huku akitikisa kichwa. "Kwa hiyo, anakufata, au mnakutana sehemu?" akamuuliza.
"Ananifata," Blandina akajibu kwa nyodo fulani hivi.
"Wacha! Malkia," Namouih akasema.
"Hahaaa... usiulize," Blandina akanena huku akirudisha nywele zake kwa nyuma kimaringo.
Wawili hawa wakaanza kucheka kwa pamoja, naye Blandina akazungukia upande mwingine wa gari na wote kuingia huku wanapiga story zenye kufurahisha. Namouih akampeleka Blandina kule alikoishi, yaani nyumbani kwa Blandina, baada ya kupata chakula kidogo kwenye mgahawa fulani, nao wakaagana kwa muda huo mpaka wakati ambao wangeonana tena jioni kwa sababu Namouih alihitaji kwenda kwake kumwandalia rafiki yake mambo mazuri kwa ajili ya kukutanika kwao baadaye.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments