MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA NANE
★★★★★★★★★★★★★
Nikiwa nahitaji kuelewa yaliyotokea hapo nje, nikaamua kurudi ndani na kuvaa suruali kabisa, kisha nikachukua mswaki na kwenda kuitoa harufu ya pombe upesi nami nikarudi ndani na kujiweka sawa. Nikatoka mpaka pale nje ya geti letu kukuta watu na watoto wamekusanyika, hasa majirani wa karibu na eneo hilo. Nadhani baadhi ya watu wa hapo walifikiri nimetoka kuja kutazama yaliyoendelea nje na kubaki kuwa mtazamaji tu, lakini nilipoona kilichoendelea hapo, sikutaka kubaki kuwa mtazamaji tu. Usawa wa geti la nyumba ya kina Tesha, walisimama watu wake wa familia, yaani mama mkubwa mweusi, Zawadi mweupe, Shadya, pamoja na Miryam. Ni Mariam tu ndiye ambaye hakuwepo. Miryam ndiye aliyekuwa amesimama mbele zaidi, huku mama zake wakubwa wakiwa nyuma yake pamoja na Tesha, na mbele yao alisimama mwanaume fulani mweupe kiasi na mtu mzima. Huyo ndiye aliyekuwa akifoka.
Alikuwa mrefu kunifikia, mwenye ndevu nyingi kidevuni na mwili mkubwa usio wa mazoezi. Alivalia shati la mikono mifupi, suruali ya kitambaa, na kitambi kilionekana kutokeza kiasi sehemu ya tumbo lake. Miguuni alivaa sendo (sandals), na kwa kumtazama tu upesi niliona alikuwa na aina fulani hivi ya urafu. Maneno aliyosema, yalikuwa yanaelekezewa kwa Miryam. Mwanamke huyo, alisimama kwa utulivu, akimtazama mwanaume huyo mbele yake kwa mkazo kiasi, nami nikapata picha fulani kwamba hawa watu walijuana. Si hata Zawadi mweupe alimwambia jamaa aingie ndani? Bila shaka walifahamiana. Lakini mpaka kuleta fujo hizo zote hapo ilimaanisha mwamba alikuwa ametibuliwa kupita kiasi na hiyo familia, nami nikawa nimemwona Ankia. Akiwa amesimama mbele yangu kiasi, nikamsogelea na kusimama karibu naye pia, naye akanitazama.
"JC... umeamka?" akaniuliza hivyo.
Nikamtikisia tu kichwa kukubali na kuendelea kumtazama mwanaume yule.
"Kwa nini hutaki? Eh? Mpaka nimelifikisha hili suala mahakamani. Jamani!" mwanaume huyo akamwambia hivyo Miryam.
"Ni haki yake! Kwa nini unalazimisha kuichukua? Ulizonazo hazikutoshi au?" Miryam akamuuliza hivyo kwa mkazo.
"Usiniletee masuala ya kusema haki, hujui haki ni nini wewe. Huyo mtoto ni kichaa, hawezi kusimamia mali chini ya hali yake hivyo ni lazima msimamizi wake halali amsaidie. Wewe una uhalali gani?" mwanaume huyo akamuuliza.
"Mimi ni dada yake..."
"Dada kitu gani? Dada nusu? Huna lolote wewe! Unakamia mali za wadogo wako halafu hufanyii lolote la maana ila kuwanunulia mapombe tu na kufanya umalaya..."
"Joshu!" Zawadi mweupe akamwita hivyo kiukali.
"Eee mama... tulia. Kwenye ukweli lazima niseme. Kwani unafikiri watu hawakujui Miryam? Hutu tucheni, tusaa, kila kitu unanyonya tu hapa, unajifanya unaweza saaana hadi kuhandle mambo ya wanaume lakini hauwezi. Wewe ni mwanamke tu!" huyo mwanaume akasema hivyo.
Nilimwangalia Miryam na kuona akijikaza sana kutolia, akiwa amekunja viganja vyake na kifua kikipanda na kushuka taratibu tu lakini kwa pumzi tetemeshi. Ni wazi maneno ya mwanaume huyo yalimuumiza, nami nikamtazama Ankia na kumuuliza, "Huyu mbwa ni nani?"
"Ni... ndugu yao sijui..." Ankia akajibu hivyo.
"Jamani... kiiila mtu anakuona kama Malaika hapa, lakini mimi ndiyo nakujua. Watu msishangae, huyu mwanamke siyo..." jamaa akaendelea kumponda Miryam.
"Unavyofanya siyo vizuri," Tesha akamwambia hivyo kwa sauti isiyo kuu sana.
"Funga mdomo wako dogo, n'takuwasha!" jamaa akamtisha namna hiyo.
Tesha akatulia. Ilionekana kama vile walikuwa wanamwogopa.
"Joshu hebu acha jamani... acha. Inakupa faida gani kumfedhehesha mwenzio?" mama mkubwa mweusi akamwambia jamaa.
"Fedheha? Hajaijua bado, leo kaionja. Wewe... nisikilize. Unaiona hii?"
Mwanaume huyo akamuuliza Miryam hivyo huku akimnyooshea karatasi fulani lililochapishiwa maandishi yaliyoonekana kuwa maalumu, naye Miryam akaendelea kumwangalia tu.
"Mimi kila kitu nimeshakamilisha, na mahakama imetoa ruhusa... hii hapa karatasi! Ukitaka soma. Lakini hapa ni moja tu. We' si ndiyo unajifanya msimamizi eh? Saini hapa kukubali nikichukue. Ukikataa... tutaonana mahakamani. Faini inakuhusu, na bado utakiachia tu..." mwanaume huyo akamwambia hivyo Miryam.
"Kaka, mbona fujo namna hiyo? Amekufanyaje?" mzee mmoja akamuuliza hivyo.
"Aa mzee, tulia. Wacha nidili naye mimi, tunajuana. Miryam... usijisahaulishe. Shika usaini..."
"Lakini kwa nini uko hivi? Tumekukosea wapi? Kweli unaamua kunifanya nionekane mbaya mbele ya jamii? Hauna hata heshima kidogo tu kwa mama zetu hawa? Hata tu huruma kumwelekea Mariam?" Miryam akaongea hivyo kwa hisia.
"Itasaidia nini? Mimi nafanya hivi ili upumue, wewe haujali lolote lile ila kuwa hapa, si ndiyo? Mariam yuko hapa, hutaki hata aende hospitali ya vichaa... si ndiyo? Umeshinda. Basi angalau itoe na hii kitu niibebe mimi na siyo kukaa tu kuiacha huko mwishowe wajimilikishe wengine..."
"Una uhakika gani siiangalii?"
"Eeee acha mdomo sana. Shika. Saini, niondoke. Usipotaka... karatasi yenyewe inaeleza... utaenda mahabusu kula busu za wajinga wenzio. Lakini tufike hadi huko ili iweje? Saini nikuondolee kelele, la sivyo... ehe!"
Nilimwangalia Miryam na kuona jinsi alivyotetereshwa sana na hali hiyo, na kuona hadi Shadya mwenye maneno mengi yuko kimya ilimaanisha alitetemeshwa sana na jamaa pia. Mama zake wakubwa na Miryam wakawa wanamshika mabegani mwanamke huyo kwa njia ya kumpa kitulizo, na huyo mwanaume, "Joshu," akamshikisha Miryam karatasi hiyo na kumpa kalamu kwa mkono mwingine.
"Unajifanya unapenda maendeleo mtu mpaka leo unaendesha kigari uchwara cha miaka nenda rudi... saini hapo..." mwanaume huyo akaongea hivyo kwa dharau na kuvuta ulimi wake ndani ya mdomo.
Alinikera. Lawama zote alizomrushia Miryam hazikuonekana kuwa za haki, na kuna kitu kilichonisukuma niamini kwamba mwanamke huyo alikuwa anaonewa. Sijui lengo lake jamaa lilikuwa kupata nini, na Mariam alihusika vipi na hayo yote, lakini fedheha alizozitoa hadi mbele ya mama wakubwa zilinichukiza sana, sana, nami nikatoka hapo nilipokuwa nimesimama na kwenda mpaka pale aliposimama Miryam. Watu waliniangalia, na huyo jamaa akanitazama pia. Sikuwa nikimwangalia yeye hata kidogo, bali macho yangu yalikuwa kwa Miryam. Mwanamke huyu akaniangalia machoni, nami niliweza kuona wimbi zito la machozi lililozuiwa kutoka kwenye macho yake ili lisilowanishe ngozi ya mashavu yake, nami nikaichukua karatasi ambayo huyo jamaa alimshikisha kwa lazima na kuitazama.
"Wewe ni nani?" akaniuliza hivyo.
Nikamwangalia kwa ufupi, kisha nikasema, "Naitwa JC. Mimi ni daktari wake Mariam."
Nikaitazama tena karatasi hiyo. Nadhani niliwaacha wengine wakinishangaa kiasi, hata Miryam akawa ananitazama kimaswali.
"Nini? Daktari wa... Miryam nini hiki?" mwanaume huyo akauliza.
"Joshua... nakuomba twende ndani tuongee... hizo hasira zako zina...."
"Hujanijibu mjinga wewe! Huyu ni nani?" jamaa akafoka.
Niliendelea kuisoma tu karatasi ile kwa umakini, lakini pia nikisikia vizuri kashfa zake.
"Joshu hebu kuwa mstaarabu... ona mpaka polisi jamii wanakuja sasa..." Shadya akasema hivyo.
"Acha waje tu! Ndiyo vizuri. Wewe... nimekuuliza huyu ni nani? Unataka kunichezea, si ndiyo?" Joshua, akauliza hivyo kumwelekea Miryam.
"Kwa nini hutaki kunielewa? Kwa nini umekuwa hivi?" Miryam akamuuliza hivyo.
"Wewe ndiyo huelewi! Una wazimu? Umeanza hadi kuleta watu wa ajabu.... Miryam unataka kunichokoza eh? Unataka mpaka nikupige ndiyo uelewe?" jamaa akamwambia hivyo huku akimnyooshea kidole.
"Umpige nani?" nikamuuliza hivyo na kumtazama.
Akaniangalia.
Nikamgeukia vizuri zaidi, naye Miryam akarudi nyuma kidogo na kusimama usawa wa bega langu.
"Nimpige nani inakuhusu nini, fala wewe?" jamaa akanipandishia sauti kwa maneno hayo.
"Sitajali ikimhusu mtu yeyote. Ila kama unataka kuona kuna vichaa zaidi yako... mguse huyu dada," nikamwambia hivyo kwa sauti makini.
Nilikuwa nikimtazama kwa mkazo zaidi, naye akawa ananipandisha na kunishusha kama haelewi somo vile. Nadhani kusimama kwangu imara mbele yake Miryam kulimpa Tesha ujasiri pia, kwani akaja mbele ya dada yake pia na kusimama kama vile anamlinda.
"Unanijua mimi vizuri?" huyo Joshua akaniuliza hivyo.
"Nikujue ili iweje?" nikamuuliza hivyo pia.
"Hunijui. Dogo! Dogo! Nitakuja nikufanyie kitu kibaya wewe!" akaniambia hivyo huku akinionyeshea kidole.
"Heee... tena yaani ndiyo nakisubiri sasa! Hicho kitu kibaya hicho... nakisubiri kwa hamu. Kilete," nikamwambia hivyo kwa ujasiri.
Akanikazia macho yake makubwa akiwa amekodoa kama vile ameibana haja kubwa kooni.
"Nyie, nini kinaendelea hapa?"
Swali hilo liliulizwa kwa besi yenye mamlaka, nami nikaangalia pembeni na kuwaona wanaume watatu waliovalia nguo za kiaskari za samawati pamoja na kofia, wakiwa wameshikilia aidha rungu ama bunduki. Mwingine kati yao nilimtambua upesi, wa nne yaani, ambaye hakuwa amevaa kiaskari, akiwa ni mwenyekiti yule tuliyeenda na Ankia ile juzi kule Mzinga kusaini makaratasi ya upangishwaji ofisini kwake.
"Eee mzee Hamadi, tena ni vizuri umekuja. Naona lugha niliyotumia kwa muda mrefu haijaeleweka kwa hawa watu kwa hiyo njoo unirahisishie kunyoosha maelezo..." Joshua akamwambia hivyo mwenyekiti.
Alifanya hadi kumshika begani kwa njia ya kirafiki na kumsogeza karibu nasi zaidi.
"Kuna nini hapa? Mbona naletewa taarifa umezusha fujo huku Joshua? Shida ni nini?" huyo mwenyekiti, mzee Hamadi, akamuuliza hivyo jamaa.
"Ndiyo usikilize sasa..." Joshua akasema.
"Joshu anataka kuvuruga tu amani hapa mtaani. Umeshindwa kuingia ndani tukaongea vizuri..."
"Kelele huko na wewe! Unajiongelesha nini, yanakuhusu?" Joshua akamkatisha Shadya kwa kufoka namna hiyo.
Inaonekana alikuwa na kiburi kwa sababu yawezekana mwenyekiti na watu wake walifahamiana naye vizuri, kwa hiyo alijua wangekuwa upande wake kwa chochote kile ambacho angesema au kufanya kwa sifa. Nilianza kumwangalia kwa hasira sana.
"Nimekuja kumwambia huyu Miryam, aachie kipande cha mali kilichowekewa jina la Mariam... nyie wote mnajua huyo msichana ni kichaa, atakishughulikiaje? Cha ajabu mtu mwenyewe hana hata habari nacho, kakitelekeza huko...."
"Una uhakika gani nimekitelekeza? Mbona unakuwa kama umelewa? Unalazimisha ukichukue, ni chako?" Miryam akamuuliza hivyo.
"Naona umeanza kunisemesha tena sasa kwa kiburi kwa sababu kuna haka kambwa kamesimama mbele yako... eh... eti kanakulinda. Unataka niweke wazi kwa hawa watu wote sababu ya mimi kutaka usimamizi wa hiyo mali? Ni mimi ndiyo nayestahili kuisimamia na siyo wewe! Damu yako haina usafi kamili kama damu yetu sisi wengine. Sijui unanielewa? Au unataka nifungue na kuitangaza maana ya hiyo stetimenti?" Joshua akamwambia hivyo.
Miryam akabaki kimya.
Hata mimi sikuelewa Joshua alimaanisha nini, lakini Miryam kukaa kimya ilionyesha kwamba kuna kitu kizito ambacho Joshua alikitumia kuwa kama sababu ya kuhalalisha mambo aliyokuwa akimfanyia; kama sababu halali ya kumsimanga Miryam. Ingekuwa muhimu sana kujua Joshua alikuwa nani kwenye familia hii, lakini kwa sasa, ni kero zake ndiyo zingetakiwa ziondolewe kwanza. Alijiona kuwa sahihi sana, na mimi ningemwonyesha jinsi alivyokuwa duni.
Joshua akanikwapua karatasi ile na kumwonyesha mwenyekiti, naye akasema, "Mzee Hamadi, hii hapa document ya mahakama. Imeeleza kila kitu. Uhalali ninao wa kuchukua... yaani, kusimamia hiyo sehemu, na nimeshampigia huyu kelele nyingi mno lakini haelewi mpaka tumefikishana huku sasa. We' mwenyewe si unanijua mzee wangu? Angekuwa amekubali wala hata usingeitwa hapa. Sasa kuna watu hapa... wanamjaza... upepo. Bichwa linakua, kama bitch! Amenisimamishia hadi na haka kabenteni kake eti kunirudisha nyuma. Mimi huyu?"
"Wewe! Shika adabu yako Joshu! Usifikiri tumekaa kimya tu basi utuone sisi ni wanyonge sana, hata sisi haki tunaijua..." mama mkubwa mweusi akamwambia jamaa.
"Aa kwenda huko, haki unaijua wapi wewe? Ungekuwa unafanya kazi kutoa pesa ya chakula hapa ndiyo ningesema eee... unaijua haki. Nyie si mnajua kula tu?" Joshua akamwambia hivyo.
Aisee! Hakuwa na heshima hata kidogo.
Mzee Hamadi akasema, "Sasa... mimi nashindwa kuelewa. Mmeshindwa kuongelea haya mambo vizuri mpaka kufanyiana fujo? Eh? Miryam mama... kwa nini hutaki kumpa haki yake ndugu yako?"
"Siyo ya kwake, ni ya mdogo wangu," Miryam akasema hivyo.
"Mdogo wako ni taahira, ataishikiliaje?" Joshua akasema hivyo.
"Wewe!" nikamwambia hivyo huku nikimnyooshea kidole.
"Unasemaje?" Joshua akanijibu hivyo na kutishia kunifata.
Nikapiga hatua kumfata pia, na wale maaskari wakatuzuia.
"Nyie, nyie, nyie, tutawachapa virungu sasa hivi! Acheni ujinga..." mmoja wao akasema.
"Huyu si mjingammoja anataka kujifanya anajua? Njoo nikuchubue huo uso vizuri!" Joshua akasema.
Tesha akanishika mikono ili kunivuta tuelekee ndani, kwa kuwa mama zake wakubwa walitaka tuondoke hapo nje, lakini nikaitoa mikono yake kwangu na kuendelea kusimama hapo hapo. Miryam akawa anajifuta machozi kwa kuwa alilia bila kutoa sauti.
"Aisee! Mkiendelea hivi tutafikishana pabaya! Mnanielewa? Joshua... na wewe kijana mgeni? Nawataka nyie wote twende kwenye ofisi yangu..." mzee Hamadi akasema hivyo kwa sauti ya amri.
"Hakuna haja ya kwenda ofisini mzee wangu. Naumaliza upuuzi wa huyu mwanaume hapa hapa," nikamwambia hivyo.
"Unasema nini?" Joshua akauliza.
"Hapana, nina tisini. Utaelewa tu," nikamwambia hivyo.
"Wewe... hebu acha..." Miryam akaniambia hivyo na kunishika mkononi kama kunizuia.
Nikamwangalia kwa ufupi, kisha nikamtazama tena mwenyekiti.
"Unataka kusema nini, mshenzi wewe?" Joshua akanipandishia bangi.
"Mzee Hamadi, angalia hiyo karatasi vizuri..." nikasema hivyo.
Mwenyekiti akaitazama kweli, naye akaniangalia na kusema, "Imefanyaje?"
"Unajua kwamba nyaraka za mahakama huandikwa na kupewa uthibitisho kutoka kwa hakimu au mwanasheria, si ndiyo?" nikamuuliza.
"Ndiyo najua..." Mzee Hamadi akajibu.
"We' si fala tu! Unataka uthibitisho gani? Hii hapa, hii hapa saini yake hakimu," Joshua akadakia na kutuonyesha.
"Hakimu mkuu, au hakimu mkazi?" nikamtega.
Akasita kidogo, kisha akasema, "Hakimu mkuu. Kwani unataka nini?"
"Muhuri wake uko wapi?" nikamuuliza hivyo.
Akabaki kimya.
Mwenyekiti akaitazama tena karatasi hiyo, bila shaka akiwa anautafuta muhuri, lakini najua hata yeye hangeweza kuuona. Akaniangalia.
"Hiyo document ni bandia. Kaiforge. Anataka kuhamisha haki ya mdogo wake Miryam iende kwake, na anahitaji sahihi yake Miryam akiwa kama msimamizi halali ili aende kufanya process za kutafuta document na viambatanishi halali, aiweke huko, halafu ndiyo hicho kipande cha mali akipate. Nadhani kaipata hata sahihi ya huyo hakimu anayemsemea kwa kutumia njia ya carbon tracing kucopy kutoka kwenye karatasi nyingine, lakini sahihi ya Miryam hakuweza kuipata, la sivyo angeitumia nyaraka hii sehemu rasmi kuhalalisha wizi wake bila yeyote kujua, na sehemu ya mali anayotaka angeichukua. Lakini kwa sababu hii kitu inaonekana halisi sana, ndiyo maana akaona aje hapa, afoke, Miryam aogope na kusaini, halafu aondoke, akidhani ameshashinda. Sijui unanielewa?" nikamwambia hivyo mwenyekiti.
Naweza kusema ukimya uliofata kwenye eneo hilo ulimaanisha kwamba watu walikuwa wanajaribu kuelewa kile nilichokisema, naye Miryam akawa ananitazama usoni kwa njia makini ya utambuzi.
Joshua akasema, "Bandia? Hahaha... huyu mjinga anaongea nini? Unazijua hati bandia wewe? Au unafikiri kila karatasi ni mpaka iwe na muhuri ndiyo ujue...."
"Ndiyo! Ni lazima," nikamkatisha kwa sauti kali.
Tesha akatoka nyuma yangu na kumsogelea mwenyekiti, akiiangalia karatasi hiyo kwa umakini.
"Sasa mzee wangu, minimum ya miaka ya kifungo kwa mtu anayefanya forgery kwa kujaribu kuiba mali unajua inafikia miaka mingapi? 10. Miaka, siyo usiku na mchana. Anachokifanya huyu mwanaume ni case ya wizi, na kutokea hapa tunaweza kumpeleka kituoni kumshitaki. Yes! Maana ushahidi huo hapo... akitaka kujitetea, basi atupeleke kwenye hiyo mahakama aliyofanyia makubaliano yote hayo na hakimu, waseme walimpa nyaraka hii muda gani, na kwa nini out of nowhere tu wakasahau kuweka muhuri. Si ndiyo anavyoweza akasema? Kwamba labda walisahau?" nikaongea hayo kwa sauti tulivu.
Mwenyekiti akamtazama Joshua, hata wale maaskari pia. Minong'ono mingi ikaanza kusikika kutoka kwa majirani na watu waliokuwa eneo hilo, naye Ankia akasogea mpaka karibu nami na kusimama hapo pia.
"Ni kitu kisichowezekana kwa sababu karatasi zao hubeba muhuri mkuu ulio embedded... yaani, unakuwa ndani kwa ndani. Unauona tu umevimba sehemu fulani kwenye karatasi. Muhuri wa mwanasheria mkuu ndiyo unapigwa kwa chini kutoa uthibitisho zaidi kama mheshimiwa kahusika. Wewe siyo wa kwanza kufanya hivi. Usijione mjanja. Waliokutengenezea hiyo kitu nawaelewa mno, ila bado hawajaweza kufaulu kudanganya vizuri kama ulivyodhania. Pole sana..." nikamwambia hivyo Joshua.
Mwanaume huyo alikuwa ananitazama kwa mkazo zaidi, akionekana kukasirishwa sana na mimi kwa sababu ya kumuumbua.
"Mmeona sasa? Kumbe yeye ndiyo mwizi! Mshenzi ni wewe Joshua!" Shadya akasema hivyo.
Nikawa nimemwangalia Shadya aliposema hivyo na kuwaona mama wakubwa wakiniangalia na kutabasamu, nami nikamtazama Miryam na kuona amekaza macho yake kumwelekea Joshua.
"Joshua, yote haya anayoyasema ni kweli. Hii karatasi ni feki. Kwa nini unafanya hivi halafu unaleta usumbufu wako huku?" Mwenyekiti akamuuliza.
Jamaa alionekana kukosa amani, lakini akasema, "Hamna bwana, walisahau tu kuweka...."
"Twendeni basi wote huko ulikoitoa hii, sawa? Sawa?" mmoja wa maaskari akamuuliza.
"Eee, mwendeni, awapeleke. Mkikuta kweli, basi sisi ndiyo wabaya. Ila mkikuta anadanganya, awekwe jela!" Shadya akaanza kuongea sasa.
"Mzee Hamadi nisikilize, unanijua vizuri...."
"Acha mambo yako ya unanijua vizuri! Unazingua! Mtu gani wewe huridhiki na yote uliyopewa unataka kubeba hadi na vya wenzako kwa visingizio visivyo na kichwa wala makalio?" Shadya akasema hivyo.
"Mbona hupayuki sasa hivi? Ongea tukusikie," Tesha akamwambia hivyo kwa ujasiri.
"Kwa hiyo dogo na wewe unanisemesha hivyo?" Joshua akamuuliza.
"Ndiyo nakusemesha hivyo. We' ni mwizi tu, hauna kazi za kufanya unakuja kufatilia tunavyoishi, si ulijitenga mwenyewe? Tunavyoishi sisi inakuhusu nini? Anavyotutunza da' Mimi ni mara milioni vizuri zaidi ya wewe unavyoweza kuitunza familia yako hata uwe na pesa ngapi. Hauwezi kumfikia. Kinachokuuma ni wivu tu kwa sababu yeye ni bora kuliko wewe. Unataka hadi kumwibia Mariam, amekukosea nini?" Tesha akamwambia hivyo kwa hisia.
Kwa jinsi Tesha alivyoongea, nilielewa hawa watu wangekuwa na uhusiano wa karibu wa kifamilia, na bila shaka Joshua alikuwa amefanya mengi mno yaliyowachukiza ndugu zake. Hata jambo hili kiukweli lilichukiza sana. Joshua akawa anamwangalia Tesha kwa njia ya hasira.
"Basi Tesha. Naomba uje huku," Miryam akamwambia hivyo mdogo wake.
Tesha akatii na kurudi nyuma ya dada yake tena.
Polisi jamii mmoja akamkamata Joshua kwenye mkanda wa suruali yake na kusema, "Tunakupeleka kituoni kabisa wewe... unatuletea kelele halafu we' ndo' mwizi!"
"Aaaa mambo gani hayo bwana? Mzee Hamadi, hivi vitu vinaongeleka... mimi sijafanya makusudi... watakuwa walikosea tu... Miryam, haikuwa... usielewe vibaya, yaani..." jamaa akashusha sauti na kuongea hivyo.
"Hivi we' ni mshenzi eti? Umekuja hapa, tunakwambia uingie ndani tuzungumze ukakataa, sa'hivi ndiyo unajifanya mtakatifu? Mpelekeni kituoni! Na sisi tunakuja. Unatuona hatujasoma eti? Leo limekutoka mpuuzi wewe!" Shadya akasema hivyo kwa hasira.
"Basi dada, inatosha..." mama mkubwa mweusi akamwambia.
"Joshua umeharibu sana unajua? Umemharibia ndugu yako taswira yake ili tu umwibie? Nadhani kama mgeombana vizuri mngeyamaliza, sasa hapa umepata faida gani? Aibu inarudi kuwa kwako..." Mwenyekiti akamwambia hivyo.
Joshua akaangalia chini kiasi, kisha akanitazama kwa njia yenye hasira. Alionekana kuwa na kiburi bado, lakini hapo ujanja ulikuwa umeshamtoka. Sikuwa hata na chembe yoyote ile ya hofu kumwelekea, zaidi nilimwona kuwa mtu anayetia huruma sana.
Mzee Hamadi akatugeukia mimi na Miryam, naye akasema, "Tunahitaji kuongelea haya mambo vizuri. Kama ni adhabu tujue nani anaipata na ifike mpaka wapi. Kijana, shukrani ziende kwako kwa kuona hilo suala la wizi maana... tungemfanyia dada wa watu vibaya. Joshua lazima ufundishwe somo, na linaanzia huku huku."
Shadya pamoja na watu kadhaa waliokuwepo wakawa wanatoa maneno ya kumuunga mkono mwenyekiti.
"Tunaenda pale ofisini, kwa hiyo... wewe dada, Miryam, watu wako wa familia mnaweza kuja pia. Na wewe kijana uje pia. Sawa?" mwenyekiti akasema hivyo.
Nikatikisa kichwa kukubali, naye Zawadi mweupe akasema, "Sawa. Tunakuja. Inabidi tujiweke sawa kwanza, sijui kama mtatusubiri..."
"Aa nyie fanyeni mnachotaka, vaeni, njooni. Sisi tunatangulia na huyu. Twende," mwenyekiti akasema hivyo.
Polisi jamii wakaanza kumwongoza Joshua kuondoka eneo hilo, huku watu wakiwasindikiza kwa macho na maneno mengi yakizungumzwa.
Mama mkubwa mweusi akamsogelea Miryam, hata na Ankia pia, nao wakamshika na kumpa pole, kisha wakaingia pamoja naye ndani ya geti lao pamoja na Shadya na Zawadi mweupe. Tesha akanionyesha ishara kwa kichwa kuwa niende huko ndani pia, nami nikampita na kuingia kabla yake. Ndani ya geti hapo nje, nikakuta Ankia akiwa amesimama kwa kuliegamia gari la Miryam, pamoja na mwanamke huyo ambaye aliliegamia pia huku akiwa ameweka kiganja chake juu ya paji la uso wake. Miryam alionekana kuvunjika moyo sana, na ni Shadya ndiye ambaye hakuacha kuzitoa kero zake moyoni kwa kuongea maneno mengi sana juu ya yote yaliyotokea. Alikuwa anampampu Miryam aende huko kwenye ofisi ya kata na kuhakikisha anamfunga Joshua, nami nikasimama tu na kuwaangalia wanawake hao wote.
"Shadya, basi inatosha. Kama ni kwenda, twendeni. Dada..." Tesha, akiwa amesimama karibu nami, akasema hivyo kwa sauti ya upole.
Miryam akawa amefumba macho bado.
"Mimi... twende mama. Mzee Hamadi hatasubiri sana unajua..." Zawadi mweupe akamwambia hivyo.
"Hapana ma' mkubwa. Nyie mbaki hapa na Mariam. Nitaenda mimi," Miryam akasema hivyo.
Alitoa jibu hilo bila kunyanyua uso, nami nilimwonea huruma sana.
Mama wakubwa wakaangaliana pamoja na Shadya pia, naye Ankia akasema, "Yuko sahihi. Bi Zawadi, Bi Jamila, mbaki na Mamu sisi tukienda huko. Tutawajulisha yaliyojiri."
"Ni sawa," mama mkubwa mweusi akamwambia hivyo.
Angalau sasa nikawa nimejua anaitwa Bi Jamila, maana mama mkubwa mweusi haikufaa kabisa kuwa jina la kumwita!
Tesha akasema, "Da' Mimi usihofu. Nenda tu kajiandae, twende tukakiwashe huko. JC ndo' mwanasheria wetu hapa. Oy, umefanya la maana sana kuja kukaa huku la sivyo huyo mjinga angetuburuza kwa hii kitu vibaya sana. Twende ukampe vyake vingine."
"Hapana..." Miryam akasema hivyo.
Wote walimwangalia, mimi pia, naye sasa alikuwa amenyanyua uso wake.
"Haina haja ya wewe kuja. Tesha... kachukue funguo utoe gari nje, nitakukuta," Miryam akasema hivyo.
Aliongea hayo bila kunitazama kabisa, naye akaanza kuelekea ndani. Inaonekana wengine walimshangaa kiasi maana waliniangalia kimaswali, naye Ankia akamshika Miryam mkono kuzuia hatua zake. Akasimama na kumgeukia.
"Miryam... JC ndiyo amesaidia mpaka huyo Joshua akajulikana, ni... muhimu aende pia," Ankia akamwambia hivyo.
"Ndiyo, hata mwenyekiti amesema... ni lazima aende..." Bi Zawadi akamwambia.
"Siyo lazima... ni... ni suala la kifamilia, nitadili nalo mwenyewe. Tesha..." Miryam akaongea hivyo.
Nilikuwa namtazama kwa umakini tu, naye akaniangalia machoni kwa ufupi, kisha akageuka na kwenda ndani. Tesha akanishika begani na kuelekea huko ndani pia, naye Ankia akaniangalia kwa hisia.
Bi Jamila, yaani mama mkubwa mweusi, akanifata taratibu na kuja kuvishika viganja vyangu kwa pamoja, naye akaniambia, "Nakushukuru sana kijana wangu. Wewe ni baraka kwetu, na hata Mimi anathamini msaada wako. Uzidi kubarikiwa."
Nikatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kuonyesha uelewa.
"Asante sana JC. Sijui vijana, mambo yenu siku hizi ni mengi ila nitakutafutia zawadi nzuri sana," Bi Zawadi mweupe akaniambia.
Shadya akacheka kidogo kwa furaha.
Ankia akaja niliposimama na kusema, "Sisi twende sasa. Miryam anaonekana atadili na hiyo ishu vizuri, kwa hiyo... JC... twende."
"Sawa. Asanteni mama zangu. Tutaonana baadaye," nikasema hivyo.
Wote wakawa wamekubali maneno yangu, nami nikageuka tu na kutoka ndani hapo pamoja na Ankia. Baadhi ya majirani waliokuwa nje walitutazama sana, na mimi nilikuwa nimeweka uso makini tu mpaka tulipofika ndani ya nyumba ya Ankia.
Kiukweli kuna vitu vingi vilikuwa vimeanza kuingia akilini hasa kwa kuunganisha matukio yote toka nilipofika na kuifahamu familia yake Miryam. Ilionekana kuwa na mambo mengi mno ambayo Ankia alikuwa ameniambia juzi hapo, japo si kwa undani sana. Sijui kwa nini lakini ingawa Miryam alionekana kutotaka nijiingize zaidi katika masuala yaliyoihusu familia yake, bado kuna kitu kilichokuwa kinanisukuma niendelee kujali; na nafikiri sehemu kubwa ya kitu hicho ilihusiana na Mariam, mdogo wake. Kuna mambo mengi yalimzunguka yule binti, na mimi kiukweli singekaa tu na kuamua kumpotezea kabisa. Hapana. Yule binti alikuwa amefanikiwa kuingia kwenye orodha yangu ya mambo muhimu ya kufatilia, na ningehakikisha natembea naye kwa ukaribu mpaka niweze kuelewa yote yaliyozunguka kwenye maisha yake, ili niweze kumsaidia.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA
★★★★★★★★★★
Comments