Reader Settings

Unaweza kurudi ulipoishia kupitia Maktaba.

INVISIBLE

A Story by Elton Tonny

Kazi, Urafiki, Mapenzi, Mahaba, Unyanyasaji, Mauaji, Mambo Yasiyotazamiwa

R-rated 18+

Enjoy!


★★★★★★★★★★★★

 SEHEMU YA SABA

★★★★★★★★★★★★


Nilishangaa sana. Baada ya wale maaskari wengine kumuuliza anamaanisha nini, alinyanyua wallet ya yule kiongozi wa wale jamaa na kuwaonyesha kitambulisho chake cha uaskari. Wote waliangaliana na kuwatazama tena hao jamaa kwa umakini.

"Ndo' nilichokuwa nataka kuwaambia bwana. Sisi ni polisi," akasema yule jamaa aliyewaongoza.

Wale maaskari waliowashikilia wakaanza kuwaachia, kisha mmoja wao akawauliza walikuwa wanafanya nini hapo. 

"Tuko kiupelelezi kutokea kitengo cha Kamishna. Kuna mhalifu hapa tunamfatilia."

Baada ya kusikia hivyo, sasa nilijua mpango wangu uliharibika. Mhalifu aliyemsemea bila shaka alimaanisha ni Malik, na kama angewaambia tu maaskari wale wamkamate na wasiamini chochote anachosema, wangefanya hivyo. 

Nikajitoa pale nilipokuwa nimesimama na kumfata Malik, ambaye alikuwa amepigwa na butwaa pia, kisha nikamvuta mikono na kumwambia, "Twende bro, tuondoke."

Alionyesha sura ya kuchanganyikiwa aliponitazama, nami nikajua hiyo ilikuwa kwa sababu hakunifahamu. 

"Mimi niko hapa kukusaidia. Wewe na mke wako... na William," nikamwambia ili kumhakikishia.

Alitikisa kichwa kukubali na sote tukaanza kuondoka taratibu ili tutafute sehemu ya kutokea. Ilikuwa wakati tulipokaribia usawa wa ngazi zilizopanda kuelekea juu, pale yule jamaa alipotuona. 

"Yule pale!" alisema hivyo huku akitunyooshea vidole na kisha kumnyang'anya bastola askari bastola yake iliyochukuliwa.

Hapa hatungeweza kukimbia mpaka kwenye mlango wa kutokea, kwa kuwa ulikuwa mbali. Baada ya kushtushwa na sauti ya huyo jamaa, nilimvuta Malik mkono nikizielekea ngazi kwa kasi sana, naye akawa nyuma yangu tukizipanda pamoja. Nilijua bila shaka tungekuwa tukifuatwa nyuma na wale jamaa; labda hata na maaskari wale pia. 

Sikuwa na muda wa kusimama, niliendelea kupanda ngazi haraka sana huku Malik akiwa nyuma yangu, na sasa nilisikia sauti nzito ya mlio wa risasi nyuma yangu iliyonifanya nishtuke sana. Nilitazama chini kidogo na kuona yule jamaa akiwa ametuelekezea bastola, hivyo kwa haraka nikamvuta Malik na kujibanza kwenye ukuta, na hapo hapo risasi nyingine ilipiga na kutoboa ukuta karibu yetu!

Sasa tulikuwa tumekoswa-koswa na risasi mbili. Mapigo ya moyo yalikimbia sana. Ilikuwa ngumu kufikiria jambo la kufanya kwa kuwa nilijua hao jamaa walikuwa wakitukaribia. Nikamwambia Malik kwa haraka 'twende,' kisha tukaendelea kuzipanda ngazi zile. Nilisikia sauti nyingi za watu wakipiga kelele, labda kwa sababu ya milio ile ya risasi, na sasa nilielewa tulikuwa tunakaribia kufika juu ya dari la ghorofa (terrace). Kuna baadhi ya watu ambao tulipishana nao wakikimbia-kimbia, na kwa bahati mbaya mmoja wao alipamiana na Malik na kusababisha amwangushe chini. 

Nikageuka nyuma na kumwona Malik akiwa anahangaika kujinyanyua, huku mkono wake mmoja ukiubana vyema mfuko ule alioushikilia. Nikarudi hatua chache ili kumsaidia anyanyuke na papo hapo, sauti ya risasi ikasikika kwa nguvu sana kwenye masikio yangu. Malik aliniangukia kifuani na kuanza kulegea. Sikuamini kilichokuwa kimetokea! 

Nilipomtazama tumboni, niliona damu zikivia shati lake la blue-bahari alilokuwa amevaa. Nilichoka. Risasi iliyopigwa, ilikuwa imempata mgongoni na kumtoboa kufikia sehemu ya mbele ya tumbo lake.

Nikiwa sijui bado la kufanya, nilihisi mikono yangu ikikabidhiwa kitu fulani. Alikuwa ananipa ule mzigo, kisha akasema, "Kimbia mdogo wangu... agh... mwokoe mwanangu..." 

Nilichanganyikiwa nisijue jinsi ya kuitikia hali hiyo. Alifanya kama kunisukuma nyuma ili kunikumbusha kuwa nilipaswa kuwahi. Nikaanza kutoka hapo mbio na kuelekea kule juu. Nilikuwa na presha sana. Kitendo tu cha mimi kumfatilia kidogo jamaa yule pale shuleni kikanipelekea kuingia kwenye kisa cha mauaji. Siku yangu ilikuwa imebadilika rangi ghafla. 

Niliendelea kupanda ngazi kwa uharaka na kufika mwisho, huku mzigo ule ukiwa bado mkononi mwangu. Nikaufungua mlango wa mwisho wa ngazi zile na kutokezea juu zaidi ya ghorofa. Kulikuwa na makolokolo mengi na madumu ya maji na pipa kubwa jeusi. Nilikosa pa kwenda. Nikasikia vishindo vya miguu vikikaribia hapo, hivyo kwa haraka nikajificha kwa kuketi nyuma ya pipa lile. 

Nilikuwa nikipumua kwa kasi sana. Nilipojiangalia kwenye shati langu, niliona rangi ya damu, iliyonikumbusha kitu kilichompata Malik muda mfupi nyuma. Mawazo yangu yote yalikuwa kwake. Nilijisikia vibaya sana na kujilaumu kwa nini sikuweza kumsaidia kwa wakati yule baba. Sauti za watu wakitembea-tembea pale juu zilisikika vizuri. Sikuwaza kugeuka nyuma kwa kuwa nilikuwa najitahidi kurudisha utulivu kwenye mwili wangu.

"Tunajua uko huku juu. Jitokeze, la sivyo utaumia..." 

Sauti ya yule jamaa ilisikika. 

"Umeona kilichompata mwenzako? Kama unajipenda bora utoke ulipojificha mdogo wangu."

Kitendo cha yeye kutumia jambo lililompata Malik kunitishia, hakikuniogopesha, bali kilinitia hasira. Nilimchukia sana mwanaume huyo. Nikifikiria mambo aliyoyafanya huku yeye akijiita polisi, ilinifanya nitake kuwa na bastola wakati huo na kufyatua bichwa lake lile. Na ni hapa ndipo akili yangu ikarudisha usawaziko ulionikumbusha kufanya kitu ambacho nilikuwa nimesahau kabisa kufanya.

"Aóratos," nikasema.

Nilifumbua macho yangu na kutazama juu kutoka nilipokuwa nimekaa na kuona mkono ukiwa na bastola mkononi ukizunguka. Kwa utulivu, niliuficha mfuko ule chini ya pipa lile kwa upande mwingine, maana nilijua ungeonwa. Bastola ile ikaelekezwa upande wangu na nikatambua aliyeishikilia alikuwa mmoja wa wale jamaa; ambao sasa hivi nimetambua kuwa siyo majambazi, ila ni mapolisi.

Hakuniona. Nilimwangalia kwa hasira sana nikiwa nimetulia hapo chini. Nilitamani nimnyang'anye bastola hiyo kisha nimmiminie risasi matakoni mwake. Lakini nilijizuia. Akatikisa kichwa chake huku anaangalia upande wa nyuma.

"Dogo amepotelea wapi?" nikasikia mmoja wao anauliza.

"Sidhani kama angeweza kuruka kutoka huku juu mpaka chini. Ametupiga chenga huyo," akasema mwingine.

"Kwani hawa watu walikuwa wamefanya nini?" nikasikia sauti hii ikiuliza hivyo na kutambua ilikuwa ni mmoja wa wale maaskari wa hapo Posta.

Yule jamaa aliyekuwa karibu yangu akaondoka, kisha nikamsikia yule jambazi-polisi akisema, "Hii kesi ni classified. Haipaswi kujulikana kwa yeyote. Tunaifatilia na kuhakikisha kwamba itamalizika haraka. Tutamfatilia huyo kijana aliyetoroka. Mwili wa huyo mwingine tutaufunga na kuondoka nao, na ikiwa mtaulizwa kama kuna mtu yeyote alikufa hapa, mkatae. Mmeelewa?"

"Ndiyo, imeeleweka," akajibu yule askari.

"Haya twendeni."

Nilibaki hapo nikiwa nimetulia tu. Nilikuwa nimechoka kiakili. Nilijawa na huzuni nilipofikiria kuhusu Malik. Lakini pia, nilijua haikuwa busara kuendelea kuketi hapo chini. Hivyo nikanyanyuka na kufikiria jambo la kufanya ili nitoke hapo. Nikauchukua mfuko ule kutoka chini. Bila shaka, mimi sikuonekana, lakini vitu nilivyobeba vilionekana, ijapokuwa sikutambua ilikuwa kwa nini nguo, simu, na viatu nilivyovaa havikuonekana nilipopotea.

Nikasogea mpaka mlangoni na kuchungulia ndani ya jengo. Sikuona mtu yeyote. Nikaingia na kuanza kushuka ngazi kurudi chini. Nilifika eneo lile nililomwacha Malik muda ule na kukuta hakuna mtu pia, wala chembe yoyote ya damu pale. Nikajua tu kuwa walikuwa wameshapasafisha. Niliendelea kwenda chini taratibu mpaka nilipofika ghorofa ya kwanza na kuona mapolisi na watu wachache eneo lile. 

Nilijua kuwa ikiwa ningepita pale, mfuko nilioubeba ungeonekana. Hivyo, nikaingia kwenye moja ya vyumba vya ofisi za mule ndani na kutafuta kitu ambacho kingeweza kunisaidia. Sikuona jambo lolote lililonipa wazo zuri hadi pale niliposogea karibu na dirisha na kuona dustbin kubwa la taka nyuma ya jengo hilo, likiwa wazi. Hakukuwa na macho yoyote upande huo, kwa hiyo nikachukua mfuko ule uliokuwa umekazwa kwa gundi za karatasi vizuri na kuurusha mpaka ukadumbukia ndani ya kopo lile. 

Nilitoka hapo haraka sana ili nielekee nje, kwa kuwa sasa sikubeba chochote ambacho kingeonwa. Nikashuka taratibu na kuwavuka mapolisi na watu wachache pale ndani, kisha kutoka ndani ya lile jengo bila yeyote kuniona. Nilipoangalia pale V8 ya Malik ilipoegeshwa, haikuwepo tena. Kulikuwa na watu wengi upande ule wa mbele, ambao bila shaka walikuwa eneo la tukio kujua mambo yaliyoendelea. Nikazunguka hadi nyuma kule kuwahi kwenye lile dustbin na kukuta mfuko ule ukiwemo bado. Nikauchukua kisha nikainama na kujibanza nyuma ya bin hilo. 

Baada ya kuhakikisha hakukuwa na mtu, nikasema, "Aóratos," kisha nikaanza kuvua shati nililovaa; ambalo lilikuwa na damu kwa mbele, na kubaki na vest nyepesi niliyokuwa nimevalia kwa ndani. Nikanyanyuka na kujitengeneza vizuri, niklitupa shati langu ndani ya dustbin kabla ya kuelekea barabarani. Nilitembea haraka sana huku natazama chini, nikiwa nimeubana mfuko ule mgumu mikononi. Nikasimamisha taxi na kuingia ndani, kisha nikamwambia dereva anipeleke maeneo ambayo niliishi.

Niliketi kwenye siti nikiwa nimefumba macho kwa dakika chache nikijaribu kuyarudia matukio ya siku hiyo kichwani mwangu. Nilijiuliza maswali mengi sana. Hawa watu walikuwa mapolisi; vipi kama Malik ndiye aliyekuwa mtu mbaya? Yeye pamoja na mke wake? Hivi kama ningeenda polisi kuwaelezea kila kitu, wangeniamini kweli? Ni upande upi uliokuwa sahihi? William alikuwa wapi? Yule dada aliendeleaje kule nilipomwacha?

Nikiwa kwenye dimbwi la maswali, nikageuza kichwa na macho yangu kudondokea mfuko ule niliokuwa nimeuweka pembeni kwenye siti. Hiki kitu kilichokuwa ndani ya huu mfuko, ndiyo kilisababisha mtoto mdogo atekwe, mama yake anyanyaswe, mume wake auwawe na mlinzi wao asiyekuwa na hatia, afe. Kikatili. Njia moja pekee ya kujua hiki kisa chote kilisababishwa na nini, ilikuwa kujua kuna nini ndani ya huo mfuko.

Nikauchukua. Ulikuwa na kauzito kiasi. Nikaanza kuzirarua gundi zile za karatasi na hatimaye, nikaufungua. Nilitoa boksi dogo la khaki lililofungwa na kisha nikalifungua. Nilipoingiza mkono na kuutoa, nilishangaa sana kuona ilikuwa ni camera. Camera ya canyon iliyokuwa na ukubwa wa wastani. Nikajiuliza wale polisi walikuwa wanamdai camera Malik, au vipi? Camera ndogo namna hii iwafanye wamuue? Ni camera ndiyo waliyoitaka, au kilichokuwa ndani ya camera?

Nikaiwasha, na baada ya kuwaka, nikaingia sehemu za kuangalia picha. Niliona picha mbalimbali za maeneo, wanyama, magari, majengo makubwa, Malik na marafiki zake na mke wa Malik pamoja na William. Walionekana kuwa watu wenye furaha sana. Nilitazama tabasamu za yule dada kwenye picha hizo, na kiukweli, zilipendeza. Alikuwa mzuri, kama mwigizaji fulani wa kihindi vile. Nikajizuia kuanza kufikiria mambo yetu yale wakati huo wa majanga, hivyo, nikabadilisha 'mode' kutoka kwenye picha kwenda kwenye video.

Video ya kwanza ilionyesha tarehe ya jana na saa kuwa saa nne asubuhi. Nikaicheza na kuanza kuona kitu ambacho kilinielezea vizuri sana hali hii yote niliyojikuta ndani yake.

Ilianza kuonyesha mwanaume fulani akiwa ameshikilia usukani wa gari akiendesha, huku sauti ya aliyeshika camera kumchukua video ikimwambia anayeendesha kuwa wamekosa matukio ya kurekodi, hivyo ataurekodi uso wake mpaka jioni. Sauti hii niliifahamu; ilikuwa sauti ya Malik. Aliyekuwa anaendesha alimtania Malik na kumwambia aache kufanya vile, lakini Malik aliendelea. Nilijiuliza ikiwa video hii ya kirafiki ingekuwa na uhusiano wowote na kisa cha sasa, lakini kwa kujua ndiyo video ya karibuni zaidi, niliamua kuendelea kuitazama tu.

Baada ya kama dakika 3 za masihara na utani kutoka kwa Malik na rafiki yake, Malik alianza kumwambia rafiki yake asimamishe gari. Alikuwa akimwambia aangalie upande fulani, na kusema kuwa pale lazima kuwe na tukio muhimu. Camera ilivuta picha kwa ukaribu lakini haikuwa safi, hivyo Malik akasema wasogeze gari karibu kidogo zaidi. Baada ya kuwa wamesogea, video ile ilianza kuonyesha watu kadhaa kwa kule mbele. Malik alishuka ndani ya gari na kusogea akinyata, huku camera ikiendelea kurekodi. 

Sasa nilianza kuwaona vizuri zaidi watu waliorekodiwa. Kulikuwa na wanaume saba wamesimama, na kuwazunguka wanaume wawili na mwanamke mmoja wakiwa wamepiga magoti. Wanaume sita waliosimama niliweza kuwatambua; ndiyo wale "mapolisi-jambazi" waliokuwa wanaitafuta camera hii ya Malik. Walikuwa wakisema vitu kama vile, wamepata hasara sana kwa sababu ya makosa ya wale waliopiga magoti pale chini. Walisema pia kwamba, kwa kuwa hao watu walijua siri zao nyingi kuhusu 'unga,' ilikuwa lazima wapotee ili kutokuja kuharibu mipango mingine.

Watu wale waliopiga magoti walikuwa wakiwaomba kwa huzuni wasiwaue. Walilia sana. Lakini, jamaa huyu-huyu aliyemteka William na kumuua baba yake, akamwangalia mtu yule wa saba aliyesimama upande wake wa kulia, kisha, mtu huyo akampa ishara kwa kichwa kukubali, na jamaa huyo akawapiga risasi wale watu watatu; kila mmoja ya kichwani. Lakini risasi zile hazikutoa kelele yoyote.

Inaonekana kitendo hicho kilimshtua Malik kwa kuwa camera ilimponyoka, na wakati anainyanyua, uso wa yule mwanaume wa saba ulikuwa ukimtazama huku akiwaamrisha wale wanaume wamkamate Malik. Malik alirudi ndani ya gari haraka huku akimwambia rafiki yake awahishe watoke eneo lile. Kisha baada ya hapo, video ikakata.

Nilifumba macho yangu na kuvuta pumzi kubwa kisha kuishusha. Sasa, nilielewa kikamili nini hasa kilikuwa kinaendelea. Watu hawa, waliokuwa wamevaa vyeo vya kulinda haki, walifanya ukosefu wa haki mkubwa sana. Waliua watu wasio na hatia kwa sababu ya tamaa zao za kijinga. Na wangeendelea kuwaumiza wengine hata zaidi ili tu wapate wanachotaka.

Kwa kuwa sasa sikuwa gizani zaidi tena, nilianza kutambua kuwa nilihitajika zaidi ya nilivyofikiri. Kwa sababu sasa camera nilikuwa nayo mimi, ningeweza kuipeleka kituo cha polisi na kuwaonyesha video ile. Lakini bado nilikuwa nikipatwa na hisi za wasiwasi. Vipi kama kwa kuipeleka kwa mapolisi ningekuwa najipeleka kwenye mtego mwingine? Kufikia hapa sikujua nimwamini nani ili anisaidie.

Niliinama na kuweka mikono yangu usoni huku nimefumba macho. Nikatafakari sana cha kufanya. Wakati nikitafakari, nilianza kukumbukia jinsi yule mwanamke alivyokuwa akipigwa, jinsi alivyolia kwa uchungu, na maneno ya mwisho ya mume wake kwangu, "mwokoe mwanangu." 

Nikanyanyua uso wangu baada ya kuiweka akili sawa, kisha nikamwambia dereva wa taxi, "Bro, naomba ugeuze tafadhali." 

Akaniuliza tunaelekea wapi. Nikamwambia nitakuwa nikimwelekeza na yeye kusema bei ingepanda. Nikamhakikishia kuwa pesa haikuwa tatizo kwa kutoa elfu 20 na kumpatia. Sasa nilichojiseti kufanya kilikuwa kitu ambacho kingebadili mchezo huu kabisa.


★★★★★★★★★

 ITAENDELEA

★★★★★★★★★

Previoua Next