MIMI NA MIMI
A Story by Elton Tonny
Familia, Urafiki, Mapenzi, Kazi, Tamaa, Hila, Usaliti, Siri, Mambo Yasiyotazamiwa
R-rated 18+
Enjoy!
★★★★★★★★★★★★★
SEHEMU YA TISA
★★★★★★★★★★★★★
Kufika sebuleni hapo nikakaa tu sofani na kumsubiri Ankia, ambaye akaingia ndani pia na kukaa sofa moja na mimi. Asubuhi hii alikuwa amevaa T-shirt kubwa la njano pamoja na khanga iliyomsitiri miguuni, na kilemba kichwani kikimpa mwonekano wake alioupenda wa 'mmama.'
"Aisee, JC! Hiyo ngoma ilikuwa ya moto!" Ankia akaniambia hivyo kwa sauti ya chini.
"Siyo kama wewe ulivyo wa moto lakini," nikamtania.
Akatabasamu kidogo.
"Umeamkia kwenye hizo fujo eh?"
"Hamna. Nimeamka, nimefanya zangu usafi hapa, ndiyo huyo mjinga akaja nilipokuwa nimemaliza tu kupika chai. Ih, af' haujanywa chai eti?"
"Usijali, niko sawa. Nitakunywa baadaye. Kwa hiyo kumbe hakuanza fujo zake zamani?"
"Hamna, yaani nimetoka nje... wewe umekuja kama baada ya dakika kumi hivi..."
"Basi inawezekana makelele yake ndiyo yameniamsha..."
"Amenikera mimi! Mimtu mingine sijui inajionaje! Amemtukana kweli dada wa watu yaani... ah! Af' eti ni ndugu kabisa..."
"Unadhani kwenye pesa kuna undugu siku hizi? I hope watamnyoosha vizuri huko huyo bwege..."
"Mimi pia. Walifunge tu. Halafu unajua nimependa sana ulivyoingilia kati huo ugomvi... vile ukasema 'ukitaka kujua kuna vichaa zaidi yako, mguse huyu dada'... yaani kama staring wa kihindi kweli! Najua lilikuogopa," Ankia akasema hivyo.
Nikatabasamu kidogo na kuangalia chini.
"Watu wote wamekuona bonge moja la msomi. Halafu hilo jitu linafikiri basi eti kila mtu angeliogopa..."
"Angejichanganya ningemfumua! Nina mkono mbaya sana Ankia, basi tu..."
"Wewe! Usinitishe mwenzio."
"Hamna, usiogope, siyo kitu yangu kupiga mwanamke. Ila wajinga-wajinga kama huyo... ingeonekana nimewashushia mpaka wakina Zawadi mweupe heshima..." nikasema.
"Zawadi mweupe? Ndiyo unamwita hivyo Bi Zawadi?" Ankia akauliza.
Nikamtazama na kutabasamu kiasi, naye akacheka kidogo.
"Aloo, ni makubwa ya leo. Ila JC... mimi naenda kukuwekea chai, hayo mengine yatajulikana yameishia wapi baadaye. Sawa?" akaniambia hivyo na kunishika begani.
Nikamkubalia kwa kutikisa kichwa, naye akanyanyuka na kwenda jikoni. Nikawa nikisikia vizuri sauti za geti lao kina Tesha na mngurumo wa gari, kuashiria kwamba Miryam ndiyo alikuwa akitoka hapo pamoja na Tesha bila shaka. Nikanyanyuka na kuelekea chumbani ili niifate simu yangu, nami nilipoichukua na kuwasha nikaona 'missed call' nne; mbili kutoka kwa yule mmiliki wa Masai bar and lodge, yaani Chalii Gonga, na nyingine kutoka kwa namba ngeni. Sikuona haja ya kuwatafuta wahusika hawa kwa wakati huu maana nilihitaji kupumzisha kwanza akili, na huyo Chalii Gonga angeniongezea tu mambo mengi akilini.
Nikaingia kwenye upande wa sms na kukuta namba ile ngeni niliyokuta imenipigia ikiwa imetuma ujumbe wa kumtambulisha mhusika, ikiwa ni Tesha. Alikuwa akiomba radhi kwa niaba ya dada yake kwa kusema Miryam alikuwa tu amevurugwa, kwa hiyo nisichukulie kwamba alikuwa amenikasirikia mimi labda mpaka kunizuia nisiende nao huko kwenye kesi iliyowahusu. Nikamjibu kifupi pia kwamba sikuchukulia vibaya, na ikiwa angehitaji msaada wangu kwa sehemu fulani kuelekea jambo hilo tena, basi asisite kunijulisha. Soraya pia alikuwa amenitumia jumbe kadhaa za kutaka tuendeleze mazungumzo. Nikamjibu kwa ujumbe pia kumwambia nilitoka kidogo, nami ningemtafuta baadaye nikishamaliza kunywa chai. Kweli nikasikia sauti ya mama mwenye nyumba wangu ikiniita nikapate chai, nami nikaelekea sebuleni kumalizana na hilo kwanza.
★★
Baada ya kumaliza kunywa chai niliendelea kukaa pamoja na Ankia sebuleni, tukitazama TV na kupiga 'story,' huku nikiwa na-chat na Soraya. Naweza kusema mwanamke huyo alikuwa amependezwa sana na mimi, lakini nilijitahidi kuweka mpaka kwenye uhusiano wetu mpya wa kirafiki tulioanzisha; kubaki marafiki. Ndiyo iliyokuwa agenda yangu. Mpaka inaingia mida ya saa saba mchana, bado nilikuwa hapo hapo sebuleni pamoja na Ankia, na ingawa nilielewa kwamba mwanamke huyu alikuwa akijaribu kunionyesha staha za kimahaba ili tufanye jambo fulani zuri pamoja, akili yangu haikuwa hapo. Bado tu nilikuwa nikimtafakari sana Mariam, na nadhani hata Ankia aliweza kuona hilo.
Tukiwa bado tumekaa kwenye sofa pamoja, akanishika begani na kusema, "JC... mbona kama una mawazo sana? Ni kuhusu hiyo ishu kwa kina Miryam?"
"Aa... yeah naweza kusema hivyo. Ila... siyo kwamba... sikuwa tu nimeitegemea..." nikamwambia.
"Hata mimi. Ila we' inaonekana kama imeku-touch mno, mpaka unakuwa hivi."
"Nakuwaje kwani?"
"Si... hadi nakutekenya kidogo lakini..."
"Lakini nini... sitekenyeki?" nikamuuliza hivyo kizembe kiasi.
Akacheka kidogo kwa haya na kuibana midomo yake.
'Usijali, niko sawa. Sema... tokea hiyo juzi... jinsi nilivyokutana na huyo dada mpaka sasa hivi yaani matukio yamejipanga kiaina fulani hivi kama yalipangwa yatokee... yaani kama kuna sababu nyingine ya mimi kuwa hapa. Sijui tu kwa nini nahisi hivyo..." nikamwambia.
"Sababu ipi sasa? Kuja kufanya ukombozi kwenye hiyo familia au? Ahahah... JC bwana," Ankia akasema hivyo kiutani.
Nikawa namwangalia tu kwa utulivu.
"Usiwe hivyo bwana. Watakuwa sawa tu. Halafu, mpigie na Tesha umuulize wamefikia wapi huko... au?"
"Hamna, siyo kuhusu fujo za Joshua..."
"Asa' ni nini JC?"
Nikatulia kidogo, kisha nikamwambia, "Nataka nikaongee na mama zao hao."
"Kuhusu nini? Familia yao?" akaniuliza.
Nikatikisa kichwa kukubali.
"Mh? Wewe sasa unataka kujiweka position mbaya, maana umeona Miryam mwenyewe hataki watu wa nje wajiingize kwenye matatizo yao. Unataka kuwasaidia kwa kipi kingine?"
"Sijui. Chochote kile," nikamwambia.
"Kwa nini?"
"Nikisema bado sijaijua sababu nitaonekana bwege, eti?"
"Hapana."
"Basi... iko hivyo tu," nikamwambia.
Akashusha pumzi na kunishika mkononi, naye akasema, "Me n'shakuelewa. Wewe ni mtu unayejali sana... na haupendi sana kuonyesha hilo, lakini nimeshaliona."
Nikatabasamu kidogo na kumbonyeza shavuni huku nikiiga ongea yake kwa kusema, "'Nimeshalioona...'"
Akacheka kidogo kwa shau.
Nikamwambia, "Ngoja niende nikazungumze nao kidogo."
"Sasa hivi? Unataka kwenda sasa hivi?"
"Ndiyo."
Akaangalia chini kiasi. Ilikuwa kwa njia ya kukwazika fulani hivi, nami nikawa nimeshamwelewa.
Nikamshika shingoni ili anitazame, na aliponiangalia nikasema, "Usijali Ankia, tutaendelea na jambo letu hata baadaye, sawa?"
"Kwa nini siyo sa'hivi?" akaniuliza hivyo kwa sauti yenye deko.
"Sa'hivi sitachangamka vizuri sana... sitaki nikupe raha kwa basi tu... nataka na mimi niihisi... na kwa sasa mawazo yako mbali. Unaelewa?"
"Mhm... haya bwana. Wewe nenda... mi' utanikuta tu," akasema hivyo.
"Sasa je! Kama msosi mtamu vile, au siyo?" nikamwambia hivyo.
Akatabasamu huku akiusugua mkono wangu taratibu.
Niliona hisia zilikuwa zimempanda mno mwanamke huyu kiasi cha kutaka kumpasua mwili, lakini kweli kwa sasa akili yangu ilikuwa imevutwa zaidi na suala la familia hiyo hapo jirani. Nikamwacha Ankia sofani na kuelekea kwa chumba, nikiwa na lengo la kwenda kuoga kwanza halafu ndiyo niende kwa mama wakubwa. Kihalisi, mpaka kufikia hatua hii ya kuamua kuongea nao ilinifanya mimi mwenyewe nitambue namna gani nilivyochukulia suala hilo kwa uzito. Na labda Ankia alikuwa sahihi kusema nilikuwa mtu mwenye kujali sana, japo ikiwa kama ningeulizwa kuhusu sehemu hiyo ya utu wangu, ningeikataa kabisa. Sababu nilizijua mwenyewe.
★★
Nilipomaliza kuoga na kuuvika mwili wangu vizuri, nikamuaga Ankia na kwenda moja kwa moja mpaka getini kwao na kina Tesha. Nikagonga geti hilo na kusubiri lifunguliwe, huku nikitambua kwamba baadhi ya watu waliokuwa nje kwenye ujirani walinitazama sana, hasa wanawake waliokaa sehemu ya ubaraza wa nyumba zao. Sikujishughulisha na utizami wa mtu yeyote kabisa mpaka mlango mdogo wa geti hilo ulipofunguliwa, na hapo nikamwona Bi Zawadi akiwa amesimama. Tabasamu mwanana likamtoka baada ya kuniona, naye akaniambia nipite ndani. Kweli nikaingia, na gari la bibie Miryam halikuwepo hapo kuonyesha bado hakuwa amerejea, naye Bi Zawadi akaufunga mlango huo wa geti na kuja usawa wangu.
"Karibu baba. Yaani hako kageti! Ingekuwa mlango wake unafungukia kwa nje ungekuwa unapita tu yaani. Sasa kuja kukufungulia inachukua muda si unajua na huu uzee hahah..." akanisemesha namna hiyo.
Nikampa tabasamu la kirafiki pia, naye akatangulia mbele yangu kuelekea ndani. Alipomaliza tu kuingia nami nikawa nimeingia, na kabla hata sijaufunga mlango, nikawa nimemwona Mariam hapo sebuleni. Mwonekano wake sasa ulikuwa tofauti kutokea ile mara ya mwisho nimemwona. Yaani, kichwani alikuwa amesukwa nywele zake kwa mtindo wa rasta nyembamba kufikia hadi mgongoni kwake, na alikuwa amevaa nguo laini aina ya Punjabi, yenye rangi mchanganyiko wa pink, nyeupe, na zambarau hasa kwenye kisuruali kilichoibana miguu yake. Kwa mara ya kwanza ndiyo nikaweza kulichora vyema umbo la mwanadada huyo mdogo, akiwa na kiuno chembamba na kalio lenye ukubwa wa kadiri, na hakuwa na tumbo wala kifua kikubwa sana. Nilichokuta anafanya sebuleni hapo kikaniacha natabasamu tu kwa sababu ya kupendezwa nacho.
Kulikuwa na wimbo wa mwanamuziki Zuchu uitwao Kwikwi, ambao ulionyeshwa kwenye TV, naye alikuwa akifatisha mitindo ya kucheza iiyoonyeshwa humo lakini kwa kuchelewa sana. Nikarudishia mlango na kuendelea kusimama hapo, huku Bi Zawadi pia akiwa amesimama usawa wa sofa na kumtazama binti huyo na tabasamu la furaha. Mariam hakuwa ameniona bado, hivyo akawa anaendelea kucheza, na cheza yake kusema kweli ilikuwa ni ya kitoto sana. Angezunguka-zunguka huku akicheka kwa pumzi, angechuchumaa huku amefunika kichwa chake kwa njia ya majonzi eti kama Zuchu, naye Bi Zawadi akawa ananiangalia huku akicheka. Ni baada tu ya wimbo huo kuisha ndiyo Mariam akatugeukia na kuniona. Nikamwonyesha tabasamu la kirafiki, lakini akaangalia chini na kuanza kufinya-finya vidole vyake akiwa ameiweka mikono yake usawa wa kiuno kwa mbele. Bi Zawadi akamsogelea karibu zaidi huku akiniambia nikae kwenye sofa, nami nikatii na kukaa. Bi Jamila akaonekana akija sebuleni hapo pia, na baada ya kuniona akatabasamu na kunisalimu vizuri, kisha naye akakaa sofa lile alilopendelea kukaa na mwenzake.
"Mariam... msalimie kaka..." Bi Zawadi akamwambia hivyo binti.
"Sh'kamoo..." Mariam akaniamkia.
Sauti yake ya usichana ilikuwa nzuri sana, lakini hakuitoa yote nje na kuongea kama anaibania kooni.
Hakunitazama kabisa usoni aliponiamkia hivyo, nami nikasema, "Marahaba mdogo wangu. Hujambo?"
Hakujibu. Akiwa bado amesimama, akanyanyua mkono wake juu kiasi na kuanza kuchezesha kidole chake kama vile anataka kukinyooshea upande fulani, lakini hata huo upande hakuuangalia kwa sababu bado alikuwa ametazama chini, huku midomo yake ikiwa inaonyesha kutaka kuongea lakini maneno yasitoke. Ilinipa picha fulani hivi juu ya mtu mwenye kuonyesha tabia za namna hiyo, na kwa haraka nikawa nimekumbuka nani. Niliwahi kuona filamu fulani ya kihindi zamani sana, iliyokuwa na mhusika mwenye umri mkubwa lakini akiwa na matendo ya kitoto yaliyosababishwa na ajali iliyompata mama yake mzazi wakati yeye bado yuko tumboni. Kumbukumbu hii ikanifanya niwaze kwamba huenda Mariam alisumbuliwa na tatizo la namna hiyo hiyo, lakini bado sikuwa na uhakika.
Bi Jamila alipoona Mariam anafanya hivyo, akamwambia, "Mamu... unataka nini? Unataka kula?"
Mariam akatikisa kichwa kukataa, huku akiendelea kufanya hivyo hivyo; miguu ikikanyaga-kanyaga chini na kufanya mwili wake ucheze, na kidole kikiwa juu bado.
"Unataka kwenda chumbani?" Bi Zawadi akamuuliza.
Mariam akavuta kichwa chake kwa njia ya kukubali.
Nikaangalia pembeni kiufupi, nikiwa naisoma tu hali yake.
"Haya, nenda mama. Ukitaka kula uje, sawa?" Bi Zawadi akamwambia.
Mariam akageuka tu na kuelekea chumbani kwa hatua za haraka-haraka, na mama wakubwa wakaniangalia kwa pamoja.
"Karibu sana JC. Ni vizuri umekuja... tena ngoja nikakupakulie..." akasema hivyo Bi Zawadi.
"Oh, hapana, asante sana mama. Bado niko fulu," nikamwambia hivyo na kutabasamu.
"Mmeshakula na Ankia eh?" akauliza Bi Jamila.
"Ndiyo. Tumekunywa chai," nikamwambia.
"Sasa chai... sasa hivi mchana bwana. Ngoja nikuwekee kande. Au hulagi kande?" akauliza Bi Zawadi.
"We! Napenda sana. Sema... chai nimekunywa muda umeenda kwa hiyo bado tumbo linaisaka pumzi. Sitatoka hapa bila kula kande lako, sawa?" nikamwambia hivyo Bi Zawadi.
Akatabasamu kidogo na kusema, "Sawa. Nimeliwekea na nazi, tamu sana. Utalipenda."
"Najua tu nitalipenda, wewe tena! Unajua mno kupika. Si unakumbuka mara ya kwanza nimekula wali wako aisee! Ni hatari..." nikasema hivyo.
Akacheka kidogo na kusema, "Umwambie huyu! Huwa ananisema eti ooh unakoseaga. Mdomo wake ushapoteza ladha ndiyo maana hajui vyakula vitamu vikoje tena."
Bi Zawadi alitumia njia fulani ya kuongea kwa mbwembwe sana, kama vile anamchamba mwenzake, na sisi tukacheka kidogo kutokana na kauli hiyo.
"Mbona huwa hata sikusemi vibaya? Nasemaga tu Mimi ndiyo fundi kuliko wote hapa, basi. We' na Shadya ndiyo mnafanya mashindano," Bi Jamila akasema.
"Kwani unafikiri Mimi alijifunzia wapi? Si kwa sisi mama zake? Mwanafunzi anaweza kumpita mwalimu kweli?" Bi Zawadi akauliza.
"Ndiyo anaweza. Mimi si huyo hapo?" Bi Jamila akamwambia.
"Miryam anajua kupika eh?" nikauliza.
"Wee! Hakuna anayemfikia, ni mwisho. Siku akiwa nyumbani hata kama amechoka vipi, wote tunategea ili aingie jikoni. Akishatenga msosi mezani yaani mpaka hautamani kuacha kula," Bi Jamila akaniambia.
"Sijakataa anajua, ila bado na mimi ni fundi. Au uwongo JC?" Bi Zawadi akaniuliza kwa njia ya kudeka eti.
Hizi "Mimi" na "mimi" kiukweli zingeweza kuchanganya mtu endapo kama asingeelewa muktadha wa kilichozungumzwa, lakini nilikuwa nimeshaanza kuzoea.
Nikatabasamu kidogo na kusema, "Hudanganyi kabisa. Hata we' ni kiboko."
Akatabasamu na kumwangalia mwenzake usoni kwa kujivuna.
"Naona Mariam anapenda muziki..." nikasema hivyo.
"Sana. Tokea zamani, anapenda sana muziki na michezo. Sema..." Bi Zawadi akaishia hapo tu na kuangalia chini.
"Matatizo mengi tu yamempata. Si unajua changamoto za maisha?" Bi Jamila akaniambia.
"Ndiyo, naelewa. Kila familia ina changamoto," nikasema hivyo.
"Ndiyo hivyo. Ila Mungu ni mkubwa, anatubariki kwa tunachopata, tunaendelea kuwa wazima, tunasonga mbele. Hata vikwazo vikija, kama hicho cha leo... tunasimama imara pamoja. Hilo ndiyo linatufanya kamwe tusikate tamaa... mengine yanajipa tu," Bi Jamila akaniambia hivyo.
Alikuwa amezungumza kwa hekima sana, busara yake kwenye maneno hayo ikionekana vizuri, nami nikaona hiyo ndiyo nafasi nzuri ya kupata kujua kuhusu hivyo "vikwazo."
Nikanyanyuka kutoka sofani, wakina mama hawa wakiwa wananitazama usoni kwa pamoja, nami nikawasogelea kufikia kwenye sofa waliloketi na kisha mimi nikashuka chini na kukaa karibu na miguu yao. Yaani nilikaa chini kabisa, karibu yao, nikiwa nimeikunjia miguu yangu katikati kama mwislamu na nikiwatazama nyusoni kwa utulivu.
Wote walionekana kunishangaa.
"JC... mbona umekaa chini baba?" akaniuliza hivyo Bi Zawadi.
"Usijali, niko sawa. Nahitaji nizungumze nanyi kwa mapana zaidi. Huwa napenda kuongea na mama yangu kwa njia hii hii pia," nikawaambia hivyo.
"Kwa nini?" akauliza Bi Jamila.
"Nimeshazoea. Ni kitu kinachonikumbusha kuwa busara yenu kama wakubwa kwangu ndiyo iko juu zaidi, kwa hiyo lazima niwatazame nikiwa chini," nikasema hivyo.
Wote kwa pamoja wakatabasamu kwa kupenda maneno hayo.
Nikiwa nimeweka uso makini, nikawaambia, "Sina muda mrefu sana toka tumefahamiana, lakini naweza kusema nyie ni watu wazuri sana. Hata mlipojua nilikosea nyumba na kuingia mpaka chumbani kwa binti yenu, hamkunitupia kashfa... bali mlinielewa. Kila mtu ana namna yake ya kuishi, na mimi nimevutiwa na nyie sana. Napenda kuwa na ukaribu nanyi... kama vile nilivyo na ukaribu na mzazi wangu."
Wote wakatikisa vichwa vyao kukubali.
"Leo hapo nje mambo hayakuwa vizuri sana... na labda nikaja kwa wakati usionifaa mimi japo nilitaka kusaidia tu... na... labda nikaongea, ama kutenda kwa njia mbaya ambayo...."
"Hapana kijana wangu, haujafanya lolote baya. Wewe umekuwa msaada mkubwa sana kwetu. Kwanza kwa nini ufikirie hivyo wakati kama usingekuja muda huo basi Miryam angejikuta anasaini bogus treaty? Haujafanya lolote baya kabisa... kuwa na amani," akaniambia hivyo Bi Zawadi.
"Nimeshakuelewa JC. Usi... usichukulie vibaya labda... jinsi Mimi alivyokuzuia usiende nao huko... najua ameonyesha kama hataki umsaidie lakini siyo hivyo..." Bi Jamila akaniambia hivyo.
Kiukweli sikuwa hata na wazo la kuchukulia vibaya kitendo cha Miryam kunizuia nisiende pamoja nao huko kwa mwenyekiti, lakini nikaona niache tu Bi Jamila aniambie maoni yake.
"Mimi huwa anapenda kushughulika na matatizo yeye mwenyewe. Yaani... ni mtu ambaye anataka afanye kazi zote peke yake, sisi tutulie tu, yeye ndiyo abebe mizigo yetu wote. Sasa... unakuta kama kwa hali kama ya leo... hivyo umemsaidia... najua anathamini, lakini naona bado anakuwa hataki mtu mwingine abebeshwe mizigo anayoona ni yeye tu ndiyo anapaswa kuibeba... yaani ndiyo yuko hivyo toka wazazi wao wote walipofariki. Umeona?" Bi Jamila akaniambia hivyo.
Nikaangalia chini na kutikisa kichwa kidogo kuonyesha uelewa.
"Ndiyo, ni kweli. Ila sisi wote tumefarijika sana ulipotusaidia... yaani! Kama msemo wa Tesha? Joshu angetuburuza sana leo kama siyo JC kumuumbua," Bi Zawadi akasema.
"Wazazi wao walikufa zamani sana?" nikawauliza.
"Hapana, si sana. Imepita tu miaka kama minne. Bado maumivu ya vifo vyao yako nasi. Ilikuwa ni kwenye ajali ya basi na... wote wakafa siku hiyo hiyo kwa pamoja," Bi Zawadi akasema hivyo kwa huzuni.
Wanawake hawa wakaangaliana kwa simanzi kiasi.
"Poleni sana," nikawaambia hivyo.
Wakarudi kunitazama tena kwa utulivu na kutikisa vichwa vyao kukubali pole yangu.
"Sawa, nimeelewa. Huwa nafurahi tu kusaidia wengine, na... wanaposaidika inafariji pia..." nikawaambia hivyo.
Wote wakatikisa vichwa vyao kukubali.
"Unajua, sisi vijana siku hizi tunafanya mambo mengi bila kufikiria matokeo yake, na yanapokuja vibaya, kujuta ni lazima, na maumivu ni lazima. Watu wazima kama nyie ndiyo mnatuongoza vizuri, kwa hiyo hata nyie mna umuhimu mkubwa sana kwenye familia yenu. Maneno ya mtu kama Joshua kuwaelekea nyinyi yasije kuwafanya mdhani labda hamna thamani katika jamii, ama kwenye familia..." nikawaambia.
"Yule kijana ni mpumbavu sana JC. Yaani... haridhikagi hata kidogo na anayopewa. Anataka tu kumharibia Miryam maisha yake na sijui ni kwa nini tu yuko hivyo!" akasema hivyo Bi Zawadi.
"Na hakuwaga hivyo. Ni basi tu... tamaa," akasema Bi Jamila.
"Kwani Joshua ni nani? Anataka nini kutoka kwa Miryam?" nikawauliza.
Wakaangaliana kwa ufupi, kisha wakanitazama tena. Nilijua huu ndiyo ungekuwa mwanzo wa kukipata kisa kilichopelekea mpaka tukio la leo kufanyika, hivyo nikaweka umakini wangu vizuri zaidi.
Bi Jamila akaanza kwa kusema, "Joshua... ni kaka yao akina Mimi..."
"Kaka? Kaka yao wa damu?" nikauliza.
"Ndiyo. Ila... Mimi amemtangulia, amemwacha kama miaka minne au mitano hivi. Akitoka Joshua ndiyo anafata Tesha na Mariam," akasema hivyo Bi Jamila.
Nikatikisa kichwa kuonyesha uelewa.
"Wamekua pamoja... Miryam ameanza kazi bado hawa wengine wako shule, lakini Joshua aliacha masomo na kuamua kuoa. Wazazi wao... walikuwa wamekusanya-kusanya mali, na unajua ingefika wakati ambao ingewabidi wazigawanye kwa watoto wao... ila Joshua akawa analazimisha apewe sehemu yake ya urithi mapema ili ndiyo akaitumie kuanzishia familia yake. Sijui ikiwa ni huyo mwanamke wake ndiyo alikuwa anamsukuma au ni yeye tu na akili zake, lakini alikuwa hasikii akiambiwa atulie kwanza.... hadi akawa anagombana na wazazi wake, shida tu ni ile kwamba yeye ni mwanaume... ana sauti... kwa hiyo wazazi wao wakaona wampe tu. Tena wakafanya kuzigawa mali zao vizuri na kwa hawa wengine wadogo ili ziwe zao kihalali na watakapofikisha umri mkubwa ndiyo wazichukue. Aliwasumbua kweli wazazi wake, yaani huyo kijana!" akasema hivyo Bi Zawadi.
"Kwa hiyo ndiyo baada ya kupewa akawa amejitenga?" nikauliza.
"Eeeh... baba yao alikuwa na mashamba kama matatu hivi... kiwanja, na duka la bidhaa. Kwenye hicho kiwanja alikuwa ameshaanza kujenga nyumba nyingine ambayo alitaka kuja kumpa Mariam, lakini Joshua akaing'ang'ania. Mama yake alikuwa ndiyo anamshawishi baba yao amwachie tu ili kuziondoa kero, kwa hiyo baba yake akampa hiyo nyumba... aliijenga huko Kongowe... unapafahamu?" Bi Zawadi akaniuliza.
"Napasikia, sijafika..." nikajibu.
"Ni hapo tu hivi mbele kutoka Mzinga, ndani ndani huko, ndiyo ipo hiyo nyumba. Akapewa na shamba moja kabisa ili asilalamike kwa lolote... na kwa sababu Tesha na Mariam walikuwa wadogo bado, wazazi wao waliona wawaandike majina yao kuwaachia mashamba mawili yaliyobaki, halafu Miryam wakamwandikia urithi wa hii nyumba na duka la baba yake. Mama yao yeye alikuwa na duka la nguo pale Mbagala pia, lakini akamwachia huyu ndugu yetu Shadya ndiyo alisimamie. Yaani... ilikuwa kama vile wamekata tamaa kwa sababu ya mambo ambayo Joshua alifanya. Karibia kila siku walipigiwa simu kuambiwa namna alivyotumia pesa kwenye starehe zilizopindukia, na hata hilo shamba alilopewa aliliuza ili apate hela ya kutumia kwa ajili ya starehe na wanawake tu..." Bi Jamila akaeleza.
"Na hapo tayari alikuwa ameoa?" nikauliza.
"Kuoa wapi JC? Mwanamke anayeishi naye mpaka sasa hivi ni wa kuweka ndani tu awe anamfulia, anampikia, anamfanyia kazi zote za nyumbani ili yeye akale tu bata. Hadi anazidiwa akili na huyu Tesha. Kasoma huko Arusha, akaanza kazi sehemu fulani huku akisaidizana na Mimi kulimisha mazao kwenye shamba aliloachiwa. Pesa akawa anapata. Sasa yeye Joshua alipoishiwa inaonekana akawa anatafuta njia ya kuzipata kutoka huku nyumbani tena... lakini hakuweza kufanikiwa maana yakwake yote alikuwa ameyamaliza kwenye upumbavu tu. Ni mtu mwenye hila sana JC. Wazazi wao walipofariki kwenye ajali... ilikuwa kama vile amefunga bao la kujisawazisha ili alete vikwazo zaidi kwenye hii familia..." Bi Jamila akaniambia hayo.
"Alifanyaje?" nikauliza.
"Alifanya ulaghai, akamwibia Tesha shamba lake... sijui alimlipa mwanasheria au nini lakini... ah! JC! Alifanya vibaya sana. Yaani hiyo akili ya wizi inaonekana yuko nayo toka zamani, maana wakaja kushangaa tu eti na shamba limeuzwa serikalini kama kiwanja kwa jina lake Tesha. Kijana akakataa kwamba hakuliuza na alishangaa sana, lakini kulirudisha haikuwezekana tena. Mimi akajaribu kufatilia mpaka akajua ni Joshua ndiyo aliyemfanyia hivyo, lakini akaona asimwambie tu Tesha maana huyu kijana ana hasira kali angeweza kufanya hata jambo baya. Tafadhali JC... usije kumwambia Tesha..." Bi Zawadi akaniambia.
"Usijali. Naelewa. Sitasema lolote kwake," nikamwambia.
"Eee... ndiyo hivyo. Tesha alikuwa na mipango yake kwenye hilo shamba masikini, huyu mpumbavu akamfanyia hivyo. Kwa hiyo Mimi akafanya mikakati kuhakikisha anazuia mambo kama hayo yasitokee tena... maana tungekuja kushtukia na hii nyumba imeuzwa. Sisi hatujakaa hapa mpaka wazazi wao walipofariki, ndiyo tukaja, na Miryam alikuwa anajitahidi kweli kusimamia vilivyoachwa na kuviangalia kwa kufanya kazi kwa bidii. Najua tu hata na shamba la Mariam huyo ng'ombe alitaka kuliiba, lakini akawa ameshindwa. Ndiyo maana akaunda hako kampango kake alikokaleta leo hapa... hajakanyaga hapa miaka... ila ndiyo kamemwotesha mapembe akafikiri na cha Mariam atakichukua. Yaani mpaka najihisi kutaka kumlaani huyo kijana!" Bi Zawadi akasema hayo na kusonya kidogo.
Wote walionekana kuwa na huzuni sana, nami niliwaelewa.
Nikawaambia, "Poleni kwa hayo yote. Ila kama wanavyosema, sikuzote za mwizi arobaini."
"Kabisa. Mimi huwa anakaa kimya tu, lakini ninajua hivi vitu huwa vinamuumiza mno. Anajitahidi sana angalau kuijenga hii familia... sawa, kuna changamoto, lakini siyo mbinafsi. Sisi tusingekuwa hapa kama asingetaka tukae. Anaona ni radhi hata asiolewe lakini mpaka ahakikishe Tesha na Mariam wamebaki katika mazingira mazuri, na salama zaidi kimaisha. Halafu eti anakuja mtu... ambaye ni ndugu yao wa damu kabisa... anatumia mpaka hali ya udhaifu ya mdogo wake ili aweze kumwibia mali... mdogo wake wa damu kabisa anamwita taahira... kweli? Huyo ni binadamu gani? Anatuambia sisi eti mmekaa kula tu hamfanyi lolote, yeye ndiyo ametuweka hapa? A-ah... hastahili kabisa kuitwa ndugu...." Bi Zawadi akasema hayo kwa hisia.
Bi Jamila akamshika mwenzake begani na kuanza kumbembeleza kwa kulisugua, maana Bi Zawadi alikuwa ameanza kutokwa hadi na machozi, nami nikatazama chini kwa huzuni. Ilinigusa sana moyoni.
"Kama nilivyosema JC... hata vikwazo vya namna hiyo vikija, tumeshajifunza kusimama pamoja kwa uimara. Umoja tulionao ndiyo unatupa nguvu ya kusonga mbele. Miryam... na wadogo zake, ndiyo nguvu yetu," Bi Jamila akaniambia.
"Poleni sana kwa kweli. Ningekuwa nayajua hayo mapema, basi... sidhani kama ningeweza kujizuia kumdunda huyo jamaa..." nikawaambia.
Wakatabasamu kwa faraja kiasi, naye Bi Zawadi akasema, "Ungemkung'uta tu. Ni mshenzi sana."
Simu yangu ikaanza kuita, nami nikaitoa na kuona mpigaji ni Chalii Gonga, hivyo nikaitolea sauti na kuiweka mezani hapo pembeni. Umakini wangu ukarudi kwa mama wakubwa.
"Mariam hakuzaliwa kama jinsi alivyo kwa sasa, si ndiyo?" nikawauliza.
"Hapana. Hakuzaliwa hivyo," Bi Zawadi akasema.
"Ilikuwaje akawa... namna hiyo?" nikauliza tena.
"Kwa kweli hatujui, yaani... Mamu amebadilika tu ghafla na kuanza kufanya vitu kama mtoto, au kichaa. Nasema kichaa kwa sababu Mimi alipompeleka hospitali walimwambia mdogo wake ana tatizo kwenye ubongo eti kwa hiyo... anatakiwa awekwe wodi za vichaa. Sisi hatumwoni kama kichaa. Mariam ni msichana mwenye akili sana, aliweza kuongea vizuri tu na kwenye masomo alijitahidi lakini eti ghafla akaanza kuwa kama bubu ama mtoto mdogo... yaani hatukuelewa..." Bi Zawadi akasema.
"Wengine wakawa wanasema amerogwa eti... mpaka Shadya akadai ni Joshua ndiyo amemfanyia hivyo maana hatupendi kweli. Hawapendi ndugu zake... anajipenda yeye mwenyewe tu. Hatuwezi kujua lakini," Bi Jamila akaniambia.
"Kwa hiyo hii imeanza kutokea akiwa mkubwa?" nikawauliza.
"Ndiyo. Alikuwa ndo' amemaliza form four. Na alifaulu vizuri. Wenye kumrushia wakamrushia," akasema hivyo Bi Jamila.
"Wazazi wake walikuwa hai bado?" nikauliza.
"Hapana. Tena... wamefariki tu hivi, ndiyo akapatwa na hiyo shida," akajibu Bi Zawadi.
"Aaa... kwa hiyo ni baada ya wazazi wake kufa ndiyo... akaanza kuwa kama haelewi-elewi?" nikauliza tena.
"Eee... ndiyo hivyo. Wamejaribu madawa, hospitali, lakini bado wanamwona kama kichaa. Kwamba anatakiwa akae na vichaa. Sisi hatutaki kumwacha huko, hasa dada yake. Mamu bado ni Mamu... na tunajua hii itapita tu. Ni kuendelea kumwomba sana Mungu, na kama kuna kitu kimefanywa hapa katikati ili kumharibia mtoto future yake... basi tunakikemea. Hizo figisu zitashindwa tu kwa uwezo wa roho ya Mungu," akasema hivyo Bi Zawadi.
Nikatazama chini kwa umakini. Nilikuwa nikitafakari yote waliyokuwa wametoka kuniambia, nami nikawa nimepata mwanga zaidi juu ya maisha ya binti Mariam.
"Vipi JC? Unawaza nini?" Bi Zawadi akaniuliza.
Nikanyanyua uso na kuwatazama.
"Unaonekana uko mbali kweli kimawazo. Tumekuhuzunisha sana, eti?" Bi Jamila akaniuliza.
"Hapana, ni... nimeguswa tu. Nawashukuru kwa kunielezea hayo yote," nikawaambia hivyo.
"Yeah, ndiyo maisha yalivyo. Hapo napo Mimi ameenda kupambana na huyo ndugu yake, kwa hiyo tusubiri kusikia nini kimetokea," Bi Jamila akasema.
"Awekwe ndani hata mwaka hivi... akili itamsogea," akasema hivyo Bi Zawadi.
"Kweli kabisa," Bi Jamila akapigia mstari.
Nikawaambia, "Cha moto atakipata tu. Ila... mimi hapa... aa... kutokana na yote mliyoniambia... kuhusu Mariam... nimeelewa sasa kinachomsumbua. Siyo kwamba Mariam amechizika, ila nadhani amepatwa na mshtuko kwenye ubongo wake. Ikiwa huo mshtuko umetikisa sehemu muhimu za kutunzia kumbukumbu za yeye kuwa nani, inasababisha utofauti utokee. Na kwa sababu siyo jambo alilozaliwa nalo... nafikiri kuna njia za kurudisha hali yake kuwa kawaida tena."
Nilipomaliza kusema hivyo, akina mama hao walikuwa wananiangalia kama vile bado walitaka niendelee kuzungumza.
"Nimeona ana njia tofauti za kuitikia mambo. Dada yake akimgusa shingoni na kumbonyeza, hata kama bado hajamwona, anajua ni Miryam. Wanapocheza rede na watoto wengine, anajua raha ipo kwenye kurusha mpira na kuponda mtu. Nilipoweka mkono wake hapa juu na kumwitikia marahabaa bila yeye kuniamkia, aliitikia kama mtoto kabisa kwa kuelewa maana ya nilichokifanya... kwamba nilikuwa namtania yeye kuwa mtoto. Mariam siyo kichaa. Ubongo wake umechanganya taarifa ulizotunza kufikia alipokuwa mkubwa na kuzirudisha nyuma, kwa hiyo anafanya mambo kama mtoto. Nadhani... ikiwa niko sahihi... kilichosababisha huo mshtuko ni maumivu aliyopata kwa kuwapoteza wazazi wake wote ndani ya siku moja. Ubongo wake haukuwa tayari kulipokea hilo... ndiyo maana yuko jinsi alivyo sasa hivi..." nikawaelezea kwa utulivu.
Wakaangaliana kwa ufupi, kisha Bi Jamila akasema, "Umeongea vizuri kweli JC."
"Sana. Mpaka umenishangaza," Bi Zawadi akasema hivyo.
Nikatabasamu kidogo.
"Umetumia muda mfupi tu kumsoma Mamu namna hiyo? Mtu hata anaweza kufikiri we' ni daktari," Bi Jamila akaniambia.
Nikaangalia chini kidogo, kisha nikamtazama kwa utulivu na kushusha pumzi.
Nafikiri Bi Jamila ndiyo akawa wa kwanza kunielewa, naye akakunja uso wake kiudadisi kiasi huku akianza kuninyooshea kidole na kuuliza, "JC... wewe ni... daktari?"
Nikatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kukubali.
Nafikiri walishangazwa na hilo, nao wakaangaliana machoni.
"Kumbe?" Bi Zawadi akaniuliza.
"Ndiyo," nikamjibu.
"Eh! Ndiyo maana kumbe uliweza kumuumbua na Joshu maana niliwaza lazima ungekuwa msomi, ila sikufikiria ni daktari kabisa," akasema hivyo Bi Zawadi.
"Unafanya kazi kwenye hospitali gani?" Bi Jamila akauliza.
"Muhimbili," nikamjibu.
Wote kwa pamoja wakatabasamu.
"Una miaka mingapi kijana wangu?" Bi Jamila akaniuliza.
"Ishirini na nane," nikamjibu hivyo.
"Aaa, nilidhani unalingana na Tesha labda, kumbe unamzidi? Na unaonekana mdogo kweli," Bi Jamila akaniambia.
"Mbona upo huku sa'hivi, hauendi kazini kwa nini?" akauliza Bi Zawadi.
"Nipo likizo fupi. Ndiyo nimekuja kupumzikia huku," nikaeleza.
"Aaa... sawa," Bi Zawadi akaonyesha kuelewa.
"Mama zangu... ninataka kumsaidia Mariam. Kwa hii miezi michache ya likizo nitakayokuwa huku, nataka niitumie kujaribu ku... cheza naye. Huenda tukaamsha kitu fulani kitakachoweza kumfanya awe sawa tena," nikawaambia hivyo kwa utulivu.
"Kweli? JC unaweza kumsaidia Mamu awe sawa tena?" Bi Zawadi akaniuliza hivyo kwa sauti yenye matumaini.
"Amesema kujaribu... siyo uhakika kwa asilimia zote, si ndiyo?" Bi Jamila akasema hivyo.
Nikatikisa kichwa kukubali, nami nikasema, "Muda ndiyo utaongea."
Wanawake hawa wakaangaliana kwa ufupi, kisha Bi Jamila akaniambia, "Sawa. Sisi hatutakuwa na neno. Ila kinachotakiwa ni wewe kuongea kwanza na Miryam. Si unakumbuka nilivyosema? Hapendi wengine washughulike na mambo anayoona kuwa ya kwake tu kushughulikia, kwa hiyo ongea naye kwanza. Na nafikiri litakuwa jambo zuri sana ukijaribu kufanya hivi kijana wangu. Tunakuamini kabisa. Na najua Mungu atakubariki kwa wema unaotuonyesha."
Bi Zawadi akanishika kichwani na kusema, "Amen katika hilo."
Nikatabasamu kidogo na kutikisa kichwa kuonyesha uelewa. Moyo ukawa umesuuzika vyema baada ya pindi hiyo iliyogusa sana hisia, si kwangu tu, bali najua hata kwa wanawake hao pia. Nilikuwa nimeshajiandaa vyema kushughulika na binti Mariam ili niweze kumsaidia kuwa na hali ya kawaida tena, lakini kwanza, ningepaswa kudili na dada yake. Na nilijua Miryam angekuwa mwenye utata kukubali msaada niliotaka kutoa, lakini ningehakikisha nautoa tu; akubali, ama akatae.
★★★★★★★★★★
ITAENDELEA...
★★★★★★★★★★
Comments